Uhusiano wa Amerika ya Kusini na Ulaya waingia mashakani
4 Julai 2013Ufaransa imeonyesha imefadhaika na kizungumkuti hiki cha kidiplomasia kilichosababishwa na kukataliwa ruhusa ndege ya rais wa Bolivia kupita katika anga ya nchi hiyo kwa dhana pengine mfichua siri anaesakwa na Marekani Edward Snowden anasafiri na ndege hiyo.
"Baadhi ya nchi za Ulaya zinabidi "zijikomboe toka milki ya Marekani ya kaskazini" lakini sisi hatuogopi kwasababu sisi ni umma huru wenye jaha."amesema rais Evo Morales alipotuwa katika uwanja wa ndege.
Jana wizara ya mambo ya nchi za nje ya Bolivia ililikataa dai la Marekani inayotaka Snowden arejeshwe nyumbani ikisema ombi hilo "linastaajabisha,si la haki na wala halina msingi."
Ufaransa yaomba radhi
Akijaribu kutuliza hali ya mambo waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Laurent Fabius alimpigia simu hapo awali waziri mwenzake wa Bolivia David Choquehuanca kumhakikishia Paris haikuwa na azma ya kuikatalia ruhusa ndege ya rais Morales kupita katika anga yake.Laurent Fabius ameelezea masikitiko ya viongozi wa Ufaransa kutokana na misuko suko iliyotokea kutokana na kukawia kutolewa ruhusa ya kuruka ndege hiyo.
Kabla ya hapo rais Francois Hollande alihakikisha "ameruhusu hapo hapo "ndege ya rais Morales ipite katika anga ya Ufaransa alipoarifiwa kwamba rais huyo wa Bolivia alikuwa ndani ya ndege hiyo.
Kisa hicho kimezusha ghadhabu nchini Boliovia na katika nchi za Latin Amerika.Kwa mujibu wa mbunge mmoja wa Bolivia,bunge la nchi hiyo linajiandaa kutaka mabalozi wa Ufaransa,Ureno na Italia wafukuzwe.Ghasia zimeripotiwa karibu na ubalozi wa Ufaransa nchini Bolivia huku bendera za Ufaransa zikichomwa moto.
Lawama za nchi za Amerika Kusini
Kisa hicho kinatishia kuzusha mzozo wa kidiplomasia kati ya Amerika ya kusini na ulaya.Washirika wa jadi wa Bolivia,Ecuador,na Venezuela,pamoja pia na Argentina,Chili na Brazil wameelezea mshikamano wao na rais Evo Morales wa Bolivia.
Viongozi wa mataifa 12 wanachama wa Umoja wa mataifa ya kusini mwa bara la Amerika wanatarajiwa kukutana leo Cochabamba nchini Bolivia kuzungumzia kisa hicho.Rais Dilma Rousseff wa Brazil ameelezea masikitiko yake kutokana na kisa hicho na kutaka nchi husika ziombe radhi.Rais Dilma Rousseff amesema kisa hicho kinahatarisha mjadala kati ya mabara mawili na uwezekano wa kuanzishwa mazungumzo kati yao.Mwenzake wa Argentina bibi Cristina Kirchner amesema kisa hicho kinakumbusha enzi za ukoloni na kwamba si tusi kwa Bolivia pekee bali kwa eneo lote la Amerika ya kusini.
Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters
Mhariri: Josephat Charo