Uhusiano wa India na Ujerumani
26 Januari 2010Hata kama uhusiano kati ya Ujerumani na India hivi sasa unanawiri, zamani haukua hivyo. Mtunga mashairi maarufu wa Ujerumani,J ohann Wolfgang von Goethe, aliwahi mnamo karne ya 19 kuusifu utamaduni na mila ya India, na hata uhusiano wa kibiashara haujaanza leo, umeanzia tangu karne ya 16. Hata hivyo, kujuana hasa nchi hizi kumeanza mwaka 1947 pale India ilipojipatia uhuru kutoka ukoloni wa Uengereza, na mwaka 1949 pale shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani lilipoundwa. Kilichoziunganisha India na Ujerumani magharibi ya zamani ni ile hamu ya kutaka kuushinda mgawanyiko wa nchi zao na kujipatia kitambulisho kipya cha kisiasa.
Waziri mkuu wa kwanza wa India, Jawaharlal Nehru, aliandika March 11 mwaka 1947 kama ifuatavyo: India haitomudu kupuuza mustakbal wa Ujerumani. Ingawa ni suala linaloihusu kwanza Ulaya, lakini linahusiana moja kwa moja, na hata kama sio moja kwa moja, na amani na kuinua hali ya uchumi ya ulimwengu mzima. Ujerumani haitoweza kujiimarisha na kufurahia ikiwa haijaungana upya.“
Hisia za Nehru za kuvutiwa mno na Ujerumani magharibi zimebainika pia kutokana na ile hali kwamba India ilikua miongoni mwa nchi za mwanzo ulimwenguni kuitambua Ujerumani mpya, kumaliza hali ya vita dhidi ya Ujerumani na kusamehe aina zote za malipo kwa uharibifu uliofanyika. Yote hayo yametokea licha ya kwamba India ilikua miongoni mwa ushirika wa nchi zilizosimama kidete dhidi ya utawala wa Hitler na pia kupotelewa na wanajeshi wake 24 elfu walioangukia mhanga wakati wa vita vikuu vya pili vya dunia.
Mnamo mwaka 1948 tayari India ilifungua wakala wa kijeshi mjini Berlin. Wakala huo ukageuka ubalozi wa India mnamo mwaka 1952. Na Nehru hakuishia hapo. Yeye binafsi na baadae binti yake, aliyeshika wadhifa wa waziri mkuu baada ya kifo chake mnamo mwaka 1964, Indira Gandhi, walipinga juhudi zote za Usovieti ya zamani na GDR kutaka GDR itambuliwe kibalozi ,hadi pale mkataba uliofafanua muongozo msingi wa Ujerumani mbili ulipokamilika mnamo mwaka 1970.
Nehru aliwahi kufika mara chungu nzima nchini Ujerumani kwa ziara za kibinafsi kabla ya India kujipatia uhuru wake. Alifanya ziara yake ya kwanza rasmi mjini Bonn mnamo mwaka 1956 na kutetea umuhimu wa kutakaswa Ulaya na silaha.
Katika enzi za vita baridi India ilifuata njia ya tatu, kundi la nchi zisizofungamana na upande wowote, licha ya kukosolewa na baadhi ya mataifa. Binafsi, Jawaharlal Nehur aliwahi kusema wakati mmoja, tunanukuu:
„ Nnataka kusema wazi wazi kabisa kwamba siasa inayofuatwa na India si siasa isiyoelemea upande wowote. Ni siasa ya maana ya nguvu inayoambatana na mapambano yetu ya kuania uhuru na mafunzo ya Mahatma Gandhis. Kwa sababu nguvu kubwa zinazotumika katika kutengeneza silaha na bajeti za nchi chungu nzima hazisaidii kudhamini amani ya dunia.“
Matukio mawili mengine yakaripuka na kuzidi kukorofisha uhusiano kati ya India na Ujerumani. Mwaka 1961 wanajeshi wa India wakalivamia koloni la zamani la Ureno, Goa, magharibi ya India. Ujerumani ilionyesha kuelemea upande wa utawala wa kiimla wa Salazar nchini Ureno na kuulaani uamuzi wa India. India ilishangazwa sana na jibu kali la nchi za magharibi. Kwa sababu kabla ya hapo juhudi zote za kuijumuisha Goa kwa njia za kidiplomasia kati ya India na Ureno zilishindwa. India ikaunga mkono vuguvugu la waliokua wakipigania uhuru mashariki ya Pakistan hadi eneo hilo lilipojipatia uhuru mnamo mwaka 1971 na kuitwa Bangladesh. Juhudi hizo pia zilikua sawa na mwiba wa mchongoma machoni mwa Ujerumani na washirika wake.
Na mengine pia yakatokea mfano pale India iliporipua bomu lake la kwanza la atomiki mnamo mwaka 1974.
Licha ya yote hayo, muungano wa Ujerumani mnamo mwaka 1990 ukageuka fursa ya kuimarika upya uhusiano wa nchi hizo mbili. Katika majukwaa ya kimataifa, India na Ujerumani zinashirikana katika mashirika tofauti ya kimataifa. India inaangaliwa kama nchi tulivu katika eneo lhilo linalogubikwa na migogoro . Na hata upande wa kiuchumi, uhusiano ni mzuri.Biashara kati ya nchi hizi mbili iliyokua ya Euro bilioni 2.7 mnamo mwaka 1990, imeongezeka na kufikia Euro bilioni 13.4 mnamo mwaka 2008. Na hata upande wa kubadilishana wanafunzi kati ya nchi hizi mbili, hali ya mambo imeimarika. Wanafunzi elfu tano wa India wanasoma nchini Ujerumani wakilinganishwa na wanafunzi 600 mnamo mwaka 1990.
Mwandishi: Hamidou Oummilkher/Yadav,Ram/ZPR
Imepitiwa na: Othman Miraji