1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Uhusiano wa Marekani na China wachukua mwelekeo mpya

Angela Mdungu
9 Julai 2023

Waziri wa fedha wa Marekani Janet Yellen amesema, mikutano kuhusu uhusiano wa China na Marekani iliyotumia saa 10 katika ziara yake imekuwa ya manufaa na yenye kusaidia kuimarisha ushirikiano wa mataifa hayo mawili.

Waziri wa fedha wa Marekani Janet Yellen na Waziri mkuu wa China Li Qiang
Waziri wa fedha wa Marekani Janet Yellen na Waziri mkuu wa China Li QiangPicha: MARK SCHIEFELBEIN/POOL/AFP/Getty Images

Ameyasema hayo wakati akikamilisha ziara yake ya siku nne Beijing. Kabla ya kuondoka China mapema Jumapili (09.07.2023), Yellen alisema kuwa nchi hizo mbili bado zinatofautiana katika masuala kadhaa lakini kuna imani kuwa safari yake hiyo imesogeza mbele juhudi za kuuweka uhusiano wa mataifa hayo katika mwelekeo sahihi.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Beijing, Yellenalieleza moja ya masuala yanayoipa wasiwasi Marekani kuwa ni kile alichokitaja kama "vitendo vya kiuchumi visivyo vya haki" na adhabu ilizozitoa dhidi ya makampuni ya Marekani.

Soma zaidi: Yellen aikosoa China kwa hatua kali dhidi ya kampuni za Marekani

Wakati uhusiano wa Marekani na China kuhusu masuala ya usalama wa taifa ukiwa dhaifu, kwa mfano, suala la Taiwan na hatua ya Marekani kupiga marufuku teknolojia na sera za viwanda zinazodhibitiwa na serikali za China, Washington imekuwa ikijaribu kurekebisha ushirikiano kati ya mataifa hayo yenye nguvu kubwa ya uchumi duniani.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony BlinkenPicha: Ichiro Ohara/The Yomiuri Shimbun/AP/picture alliance

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken, alitembelea Beijing mwezi uliopita, hiyo ikiwa ni ziara ya kwanza ya mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa utawala wa Rais Joe Biden nchini humo.

Mjumbe wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi John Kerry, naye anatarajiwa kuizuru China mwezi huu.

Soma zaidi: Yellen airai China kupambana na mabadiliko ya tabianchi

Ziara hizo za kidiplomasia zinafanyika kabla ya uwezekano wa kufanyika kwa mkutano kati ya Rais Xi Jinping na Joe Bidenwakati wa mkutano wa mwezi Septemba wa mataifa yaliyoendelea na yanayoinukia kiuchumi yanayounda kundi la G20 huko New Delhi, au kwenye mkutano wa Jumuiya ya ushirikiano wa kiuchumi wa mataifa ya Asia na Pasifiki utakaofanyika mwezi Novemba mjini San Fransisco.

Waziri wa fedha wa Marekani Janet YellenPicha: Pedro Pardo/AFP/Getty Images

Katika ziara hiyo ambayo Yellen ameitaja kuwa madhumuni yake ni kuimarisha na kukuza ushirikiano wa Marekani na timu mpya ya masuala ya uchumi ya China, ni kupunguza hatari ya kutokuelewana na kufungua njia ya kushirikiana kwenye masuala kama vile mabadiliko ya tabianchi na madeni. Hata hivyo amesema China kwa upande wake imeonesha wasiwasi kuhusu amri  inayotarajiwa ya kiutendaji inayozuia uwekezaji kutoka nje ya Marekani.

Yellen amesema kuwa aliwaambia maafisa wa serikali ya China kuwa wanaweza kuelezea hofu yao kuhusu hatua zinazochukuliwa na Marekani ili Washington izitolee maelezo.  Katika ziara yake, Yellen alipata nafasi ya kukutana na waziri mkuu Li Qiang, makamu wa waziri mkuu mwenye dhamana ya kusimamia sera za uchumi nchini humo He Lifeng. Alikutana pia na Gavana msaidizi wa benki ya China Pan Gongsheng, makampuni ya Marekani yanayofanya biashara China, wataalamu wa masuala ya fedha na wanauchumi wanawake.