Uhusiano wazidi kuporomoka Ujerumani na Uturuki
11 Septemba 2017Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Ujerumani Martin Schaefer amewaambia waandishi habari kwamba wizara hiyo imepata ishara mahsusi kwamba Wajerumani wawili , ambao ni mke na mume wake , wako mikononi mwa polisi tangu mwishoni mwa juma.
Haifahamiki watu hao wamekamatwa kwa sababu gani, lakini Schaefer ameongeza kwamba mmoja ameachiliwa huru na ameamriwa kuondoka nchini humo.
"Hii ina maana jinamizi kwa Wajerumani wengi ambao hawataki chochote zaidi ya kufurahia mapumziko yao ya likizo nchini Uturuki linaendelea," amesema.
"Hali hiyo inaweza kumuathiri mtu yeyote ambaye ataamua kusafiri kwenda Uturuki. Hutarajii hatari yoyote na ghafla unawekwa jela, hilo ni jambo la huzuni kabisa ambalo tunakabiliana nalo."
Schaefer amesema kutokana na hali hiyo ya kigeugeu ya maafisa wa Uturuki , Ujerumani inatafakari kuiweka Uturuki katika orodha ya nchi zisizo faa kwenda hapo baadae. "Iwapo hali hii itaendelea kuwa ya kila siku kwa maafisa wa Uturuki kuwakamata raia wa Ujerumani mpakani na kuwaweka korokoroni , inawezekana kwamba wakati utafika kwamba ushauri wa kusafiri utatolewa," amesema.
Uhusiano wadhoofika
Uhusiano kati ya Uturuki na Ujerumani umedhoofika tangu jaribio la mwaka jana la mapinduzi dhidi ya rais Recep Tayyip Erdogan na ukosoaji mkali wa Ujerumani uliosababishwa na ukandamizaji nchini Uturuki ambao umeshuhudia zaidi ya watu 50,000 wakikamatwa. Mahusiano yaliporomoka zaidi baada ya kukamatwa kwa raia kadhaa wa Ujerumani ikiwa ni pamoja na Deniz Yucel , mwandishi habari wa gazeti la Die Welt.
Wajerumani 11 wanashikiliwa na Uturuki kwa sasa kwa sababu za kisiasa, ikiwa ni pamoja na watatu ambao walikamatwa tangu majira ya joto mwaka jana , kwa mujibu wa wizara ya mambo ya kigeni ya Ujerumani.
Wakati huo huo kwa mujibu wa waraka uliotolewa na wizara ya uchumi ya Ujerumani, na kuonekana na shirika la habari la Ujerumani dpa serikali ya Ujerumani imeidhinisha mauzo ya silaha nchini Uturuki yenye thamani ya euro milioni 25 tangu mwanzo wa mwaka huu 2017. Silaha 99 zilipokelewa nchini Uturuki zikiwa na thamani ya euro milioni 25.36 ziliidhinishwa na serikali ya Ujerumani kati ya januari na Agusti , mwaka huu , kwa mujibu wa jibu la wizara hiyo kutokana na ombi la uhuru wa kupata taarifa kutoka chama cha upinzani cha kijani.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / rtre
Mhariri: Yusuf , Saumu