1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUingereza

UK: Bunge kujadili tena juu ya wakimbizi kupelekwa Rwanda

21 Machi 2024

Mpango wa Waziri Mkuu wa Uingereza wa kuwapeleka nchini Rwanda watu wanaotafuta hifadhi nchini humo utajadiliwa tena bungeni mara baada ya wabunge kurudi kutoka kwenye mapumziko ya sikukuu ya Pasaka.

Uingereza | Bungeni
Wajumbe ndani ya Bunge la UingerezaPicha: House of Commons/UK Parliament//PA Wire/empics/picture alliance

Sheria ambayo inalenga kuzuia hatua zaidi za kuifikisha mahakamani serikali ya Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak kuhusu mpango wake wa kuwapeleka nchini Rwanda watu wanaotafuta hifadhi nchini Uingereza itajadiliwa bungeni baada ya mapumziko ya sikukuu ya Pasaka.

Kulingana na tangazo la kiongozi wa Bunge Penny Mordaunt wabunge watalijadili swala hilo mnamo tarehe 15 mwezi ujao wa April.

Mswada huo lazima pia ujadiliwe kwenye Baraza la juu la Bunge baada ya wabunge kuupinga siku ya Jumatano - 20.03.2024. Wabunge wanataka sheria hiyo ijadiliwe na mabunge hayo mawili hadi yatakapokubaliana juu ya maneno yanayopaswa kutumika katika sheria hiyo.

Soma Pia: Mpango wa Uingereza kuwahamishia wakimbizi Rwanda kugharimu pauni milioni 300

Wajumbe wa Baraza la juu la Bunge ambao hawakuchaguliwa, wengi wao wakiwa wanasiasa wa zamani na maafisa wa serikali, walipiga kura siku ya Jumatano kwa mara ya pili kuunga mkono marekebisho ya sheria ya kuwekwa vizingiti zaidi ili kulinda haki za wanaotafuta hifadhi.

Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi SunakPicha: Jessica Taylor/UK Parliament/AFP

Serikali ya Uingereza inataka kuwapeleka nchini Rwanda maelfu ya watu wanaotafuta hifadhi nchini humo. Watu hao ni wale walioingia Uingereza kupita njia ya baharini. Hata hivyo changamoto za kisheria zimezuia hadi sasa kusafirishwa hata mtu mmoja na kupelekwa katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Ili kuondoa mapingamizi ya mahakama, serikali ya Waziri MkuuSunak inajiandaa kuupitisha mswada unaoitangaza Rwanda kuwa ni nchi salama na hivyo kuwezesha kukiruka kiunzi cha sheria ya haki za binadamu ambacho hakitaweza kutumiwa baada ya mswada huo kupitishwa. Mswaada huo unalenga kuzuia changamoto zaidi za kisheria.

Soma Pia: Sunak apata "pigo" katika kuwapeleka wahamiaji Rwanda

Wajumbe wa Baraza la juu la Bungewalipiga kura kwa ajili ya marekebisho ambayo yatawalazimu mawaziri kuzingatia sheria ya ndani na ya kimataifa na nyingine itakayoiwezesha serikali ya Uingereza kuitangaza Rwanda kuwa nchi salama wakati mkataba kati ya Uingereza na Rwanda utakapotekelezwa.

Chanzo: RTRE

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW