1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza: Chama cha Conservative chatarajiwa kushinda

Zainab Aziz Mhariri: Amina Mjahid
13 Desemba 2019

Chama cha kihafidhina cha Waziri Mkuu Boris Johnson kinaelekea kupata ushindi mzuri katika uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Uingereza kwa mara ya tatu mnamo kipindi kisochozidi miaka mitano.

UK Wahlen 2019 | Erste Hochrechnung
Picha: Getty Images/AFP/T. Akmen

Kulingana na utabiri chama hicho cha Conservertive kinatarajiwa kushinda viti 368 katika bunge lenye jumla ya viti 650. Ushindi huo utakuwa mkubwa kabisa kwa chama hicho tangu uchaguzi wa mwaka 1987 chini ya uongozi wa aliyekuwa waziri mkuu Margaret Thatcher.

Iwapo utabiri huo utathibitika Waziri mkuu Johnson ataweza kusonga mbele na ajenda ya kuiondoa Uingereza kutoka Umoja wa Ulaya. bwana Johnson ameahidi kuiondoa nchi yake kutoka kwenye jumuiya hiyo ifikapo mwishoni mwa mwezi Januari mwaka ujao.

Chama cha upinzani cha Labour kinatarajiwa kupata viti 191, kiwango hicho kinawasilisha matokeo mabaya kabisa kwa chama hicho tangu mwaka 1935. Chama cha Scottish National cha Scottland kinatarajiwa kupata viti 55 na kile cha Lib Dem kinatabiriwa kupata viti 13. Wakati kura zinapoendelea kuhesabiwa chama cha Brexit Party cha Nigel Farage kinatabiriwa kuondoka patupu.

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amesema maamuzi muhimu yatafanyika baada ya matokeo rasmi kutangazwa.

Kushoto: Kiongozi wa upinzani Jeremy Corbin. Kulia: Waziri Mkuu wa Uingereza Boris JohnsonPicha: AFP/T. Akmen/L.eal-Olivas

Ufaransa imesema ushindi wa Waziri Mkuu Boris Johnson utawezesha kutekelezwa mchakato wa Brexit kwa utaratibu mzuri. Wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya wamesifu kinachoelekea kuwa ushindi wa chama cha Conservertive katika muktadha wa mkwamo wa mchakato wa Brexit. hata hivyo waziri wa Ufaransa anayeshughulikia masuala ya Ulaya Amelie de Montchalin amesema itakuwepo chanagamoto kwenye mazungumzo ya kufikia makubaliano ya biashara na Uingereza hadi kufikia mwishoni mwa mwaka ujao wa 2020. Waziri huyo ameeleza kwamba viongozi wa Umoja wa Ulaya sasa watakuwa na mamlaka ya kuzungumzia juu ya uhusiano wa siku za usoni kati ya jumuiya ya Ulaya na Uingereza.

Bwana John MacDonnel anayeshika nafasi ya pili katika uongozi wa chama cha Labour amesema uchaguzi wa jana uligubikwa na suala la Brexit ambalo limewagawanya waingereza tangu kufanyika kura ya maoni mnamo mwaka 2016. 

Waingereza milioni 45 walistahiki kuwapigia kura wabunge 650. Licha ya baridi kali, mvua na theluji katika baadhi ya maeneo, wapiga kura walijitokeza kwa wingi ili kushiriki kwenye zoezi la kupiga kura.  kwa jumla uchaguzi huo wa jana uligubikwa na suala la Brexit lakini masuala mengine yalihusu sekta ya afya, mabadiliko ya tabia nchi na uchumi.

Wakati huo huo sarafu ya Uingereza Pound imeongezeka thamani kwa asilimia 2 kulinganisha na dola ya Marekani na asilimia 1.6 kulinganisha na sarafu ya Euro. Pauni imeongezeka thamani kutokana na utabiri wa ushindi wa chama cha Conservertive.

Vyanzo: /RTRE/AFP/AP

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW