1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza ina wasiwasi juu ya sheria mpya ya China

30 Juni 2020

Uingereza imesema ina hofu kufuatia China kupitisha sheria kali ya usalama wa taifa mjini Hong Kong huku ikisema itaangalia iwapo China imevunja mkataba wa pamoja kati ya mataifa hayo mawili.

Coronavirus | London PK Premierminister Boris Johnson
Picha: picture-alliance/empics

Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson pamoja na Waziri wa mambo ya kigeni, Dominic Raab wamesema wana wasiwasi baada ya bunge la China kuidhinisha sheria hiyo.

Wamesema wataiangalia sheria hiyo kwa makini ili kuelewa iwapo China imekiuka tamko la pamoja baina ya Uingereza na China. Akizungumza na waandishi habari Waziri Mkuu Johnson amesema watatoa majibu yao hivi karibuni baada ya kuifanyia utafiti sheria hiyo. 

Uingereza iliirejesha Hong Kongmikononi mwa China mwaka 1997 kukiwa na makubaliano kwamba itaimarisha uhuru kadhaa pamoja na uhuru wa mahakama na sheria kwa miaka 50. China inasisitiza kuwa mpango wa utawala wale wa mfumo wa taifa moja, mifumo miwili, bado unaheshimiwa, lakini wakosoaji wanaamini kwamba sheria hiyo mpya inatishia uhuru wa raia katika eneo hilo la kibiashara.

Uingereza imekuwa ikisema mara kwa mara kwamba ina wasiwasi juu ya sheria hiyo ambayo imeidhinishwa baada ya maandamano ya mwaka uliopita dhidi ya pendekezo la kukubali watuhumiwa wa uhalifu kufunguliwa mashitaka China bara. Awali Uingereza ilikubali kutoa visa kwa mamilioni ya raia wa Hong Kong iwapo sheria hiyo itapitishwa.

Raab kwa mara nyengine ameihimiza China kurejea nyuma, kuheshimu haki ya watu wa Hong Kong na kutekeleza wajibu wake wa kitaifa kupitia mkataba wa pamoja.

Carrie Lam aitetea sheria ya usalama wa taifa ya China kwenye Umoja wa Mataifa

Kiongozi wa Hong Kong Carrie LamPicha: picture-alliance/AP Photo/V. Yu

Huku hayo yakiarifiwa, kiongozi wa Hong Kong Carrie Lam, ameliambia Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa kwamba sheria hiyo itawalenga watu wachache tu kwenye jimbo lake, huku akiitolea wito jumuia ya kimataifa kuheshimu haki ya China kulinda usalama wake.

Lam ameitetea sheria hiyo iliyoidhinishwa kwa sauti moja na China, akisema ilikuwa inahitajika sana, kwani Hong Kong imekuwa ikiishi na mapungufu makubwa ya usalama wa taifa.

Carrie Lam aliliambia Baraza hilo kuwa Hong Kong ni sehemu ya China isiyotenganishika na kwamba ni jambo la ajabu kuwa wakosoaji wa sheria hiyo wanailenga China pekee kutunga sheria inayolinda kila pembe ya ardhi yake.

Chanzo: dpa

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW