1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza ipo njiani kuwapeleka wakimbizi Rwanda

20 Machi 2023

Licha ya malalamiko makubwa kutoka mashirika ya haki za binaadamu ulimwenguni, London na Kigali zinaelekea kutekeleza mpango wao wa kuwahamisha waomba hifadhi nchini Uingereza na kuwapeleka Rwanda hivi karibuni.

Großbritannien | Suella Braverman
Picha: Amanda Rose/Avalon/Photoshot/picture alliance

Serikali ya Uingereza ilisema hapo siku ya Jumapili (Machi 19) kwamba ingeliweza kuanza kuhamamishia waomba hifadhi nchini Rwanda miezi michache kutoka sasa, ikiwa mahakama zitaamua kwamba sera hiyo yenye utata ni halali kisheria.

Ripoti iliyotolewa na wizara ya mambo ya ndani ya Uingereza ilisema inakusudia kuanza safari za ndege kuwachukuwa waomba hifadhi hao kabla ya majira ya kiangazi yanayoanza hivi karibuni.

Taarifa hiyo ilitolewa wakati Waziri wa Mambo ya Ndani Suella Braverman akiitembelea Rwanda kwa lengo la kuhakikikisha utayari wa serikali ya chama cha Wahafidhina kwenye utekelezaji wa mpango huo unaopingwa vikali na makundi ya kutetea haki za binaadamu na wakimbizi duniani.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza, Suella Braverman.Picha: Jacob King/PA/picture alliance

Akiwa mjini Kigani, waziri huyo alikutana na Rais Paul Kagame na waziri wake wa mambo ya kigeni, Vincent Biruta, na pia kutembelea nyumba zinazokusudiwa kuwahifadhi wakimbizi watakaohamishiwa huko.

Soma zaidi: Waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza ziarani nchini Rwanda

Waziri Suella Braverman pia aliweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa nyumba nyengine 1,000 kwa ajili ya wahamiaji hao. "Nimejionea kwa kina na kwa jicho langu mwenyewe fursa nyingi ambazo nchi hii inaweza kuwapatia watu wanaohamishiwa hapa kupitia ushirikiano wetu." Alisema.

Rwanda yasema iko tayari

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Vincent Biruta, alisema nchi yake itawapatia wahamiaji hao fursa ya kuanzisha maisha mapya kwenye eneo salama kupitia makaazi, elimu na mafunzo ya amali.

Msemaji wa serikali ya Rwanda, Yolande Makolo, aliwaambia waandishi wa habari kwamba nchi yake iko tayari kuwapokea maelfu ya wahamiaji kutoka Uingereza, akisema hachukulii kuwa kuishi Rwanda ni adhabu.

Soma zaidi: Kagame na Sunak wazungumzia mkataba juu ya wahamiaji

"Rwanda imedhamiria kuhakikisha kuwa mpango huo unafanikiwa", aliongeza.

Uingereza na Rwanda zilifikia makubaliano takribani mwaka mmoja uliopita ambayo yanatoa ruhusa kwa baadhi ya wahamiaji wanaowasili Uingereza kwa njia haramu kuhamishiwa Rwanda, ambako maombi yao hifadhi yatashughulikiwa, na wale watakaokubaliwa hifadhi watasalia Rwanda badala ya Uingereza.

Mpango wenye utata

Serikali ya Uingereza inadai kuwa sera hiyo itavunja biashara haramu ya kusafirisha watu na kuwavunja moyo wahamiaji wanaobahatisha maisha yao kuvuuka ujia wa maji maarufu kama English Channel kuingia Uingereza.

Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak, akizungumza bungeni.Picha: PRU/AFP

Zaidi ya watu 45,000 waliwasili nchini Uingereza kwa mashua mwaka 2022, ikilinganishwa na 8,500 mwaka 2020.

Soma zaidi: Mahakama ya Uingereza yahalalisha mpango wa kupelekwa kwa wahamiaji nchini Rwanda

Hata hivyo, mpango huo wenye thamani ya paundi milioni 140 umekumbwa na mkwamo wa kisheria, na hadi sasa hakuna mkimbizi hata mmoja aliyepelekwa Rwanda. 

Mwezi Disemba, Mahakama Kuu ya Uingereza iliamua kwamba sera hiyo ni halali kisheria, lakini kundi la waomba hifadhi kutoka mataifa ya Iran, Iraq na Syria limepewa ruhusa ya kuukatia rufaa uamuzi huo.

Makundi ya haki za binaadamu yanasema kutokana na rikodi mbaya ya haki za binaadamu ya Rwanda haistahiki kuwapeleka waomba hifadhi umbali wa kilomita 6,4000 katika nchi wasiyotaka kwenda kuishi.

Vyanzo: Reuters, AP