1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza kusitisha mkataba wa kubadilishana watuhumiwa

20 Julai 2020

Serikali ya Uingereza inaangazia kuubadilisha mpango wake unaohusiana na kuwahamisha washukiwa kati yake na Hong Kong hii leo baada ya China kuanzisha sheria mpya na ngumu ya usalama.

UK Coronavirus | Boris Johnson kündigt Lockerungen an
Picha: picture-alliance/NurPhoto/W. Szymanowicz

Serikali ya Uingereza inaangazia kuubadilisha mpango wake unaohusiana na kuwahamisha washukiwa kati yake na Hong Kong hii leo, baada ya China kuanzisha sheria mpya na ngumu ya usalama katika jiji hilo ambalo ni kitovu cha biashara ulimwenguni. 

Wakati hali ya wasiwasi ikizidi kuongezeka kati ya Uingereza na Beijing, waziri mkuu Boris Johnson amesema ana hofu kuhusu sheria mpya na madai ya ukiukwaji wa haki za binaadamu nchini China na hususan namna inavyoichukulia jamii ya Waislamu walio wachache wa Uighur. Johnson aliahidi kuchukua hatua kali, lakini akisema haitamaanisha kuachana kabisa na sera ya kimahusiano na China.

Johnson amesema ataliacha suala hilo mikononi mwa waziri wa mambo ya kigeni Dominic Raab kuyaainisha mabadiliko hayo wakati atakapotoa taarifa mbele ya wabunge baadaye leo.

Dominic Raab, waziri wa mambo ya kigeni wa UingerezaPicha: picture-alliance/Photoshot/UPPA/Avalon/J. Ng

Raab hapo jana alisema suala hilo halitaendelea kuwa la kawaida tu wakati kukiripotiwa kwamba alikuwa njiani kufuata nyayo za Marekani, Australia na Canada katika taarifa yake ya baadaye za kusitisha mipango ya kubadilishana watuhumiwa na Hong Kong.

Kupitiwa upya kwa hatua hizo za mabadilishano kunakuja siku chache tu baada ya Uingereza kuupitia upya mpango wake wa kuipatia jukumu kampuni kubwa ya mawasiliano ya China, Huawei kwenye mtandao wake wa simu za mkononi huku kukiwa na wasiwasi wa kiusalama uliochochewa na kuongezeka kwa hofu kati ya Beijing na mataifa ya magharibi.   

Serikali ya Johnson tayari imekosoa vikali uamuzi wa China wa kuanzisha sheria hiyo mpya ya usalama kwa Hong Kong. Aidha imeituhumu China kwa kukiuka pakubwa mkataba kati yake ya Uingereza kuhusu Hong Kong, ambao utekelezaji wake ulihusisha makubaliano ya Uingereza kurejesha udhibiti wa Hong Kong kwa China mnamo mwaka 1997.

China inakana vikali tuhuma dhidi yake kuhusiana na namna inavowachukulia Waislamu wa UighurPicha: Getty Images/AFP/O. Kose

Hata hivyo, serikali ya Beijing imepinga vikali hatua hiyo. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya China Wang Wenbin amesema wanapinga vikali na wanaitaka Uingereza kuachana na maamuzi hayo mabaya. "Matamshi ya uongo na hatua za hivi karibuni zilizochukuliwa na Uingereza juu ya Hong Kong kwa kiasi kikubwa vinakiuka sheria za kimataifa na misingi ya kusimamia sheria za kimataifa, lakini pia kwa kiasi kikubwa kuingilia masuala ya ndani ya China. China inalaani vikali hilo na inapinga vikali. Tunaiomba Uingereza kuachana na hatua hizo potofu ili kuzuia athari zaidi kwenye mahusiano ya mataifa hayo." alisema Wenbin.

Balozi wa China nchini Uingereza Liu Xiaoming katika siku za hivi karibuni pamoja na kuielezea hatua hiyo kama uingiliaji mkubwa wa Uingereza kwenye masuala ya ndani ya China, alisema Uingereza ilikuwa inafuata tu nyayo za Marekani huku akikana madai hayo ya China kuwatendea visivyo Waislamu wa Uighur.

Wanaharakati wa haki za binaadamu na wataalamu wanakadiria zaidi ya watu milioni moja wa jamii ya Uighur, na wengi miongoni mwao wakiwa Waislamu wamezingirwa kwenye makambi ya uhamasishaji, ambayo China inadai ni makambi yanayotoa mafunzo ya ajira na kuwafunza watu hao kujiepusha na misimamo mikali.

Soma Zaidi:Ushahidi: China inawafunga Wauighur bila sababu za msingi 

Mashirika: APE/AFPE.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW