1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza kuunda kikosi cha ulinzi Ghuba

Faiz Musa 23 Julai 2019

Uingereza inapanga kuwa na kikosi maalum cha mataifa ya Ulaya kitakachokuwa kikitoa ulinzi kwa shughuli zao za usafirishaji katika bahari ya Ghuba baada ya meli ya mafuta ya Uingereza kukamatwa na serikali ya Iran

London, Jeremy Hunt spricht im Parlament NEU
Picha: AFP/PRU

Waziri wa maswala ya kigeni wa Uingereza Jeremy Hunt alisema wanapanga kuanzisha kikosi hicho kwa haraka sana huku akilieleza bunge la Uingereza kwamba kikosi hicho hakitakuwa na uhusiano na mipango ya Marekani katika kuongeza shinikizo kwa Iran maana Uingereza inataka mkataba wa makubaliano wa nuklia kutekelezwa. Jeremy aliongeza kwamba tayari meli ya pili ya kivita waliyoituma katika bahari ya Ghuba itawasili huko mwishoni mwa mwezi huu. 

"Kwa sababu uhuru wa shughuli za baharini ni muhimu kwa masilahi ya kila taifa sasa itatubidi kuungana pamoja mataifa ya ulaya na kutengeza kikosi cha ulinzi baharini ili kuhakikisha usalama wa mabaharia na mizigo katika kanda hii muhimu," alisema Jeremy.

Kwa upande wa Iran, waziri wa maswala ya kigeni Mohammed Javad Zarif alisema Iran haitafuti mgogoro na Uingereza. Javad amemjibu mwanasiasa wa ngazi ya juu nchini Uingereza Boris Johson  kwamba Iran inataka uhusiano mzuri na Uingereza kwa misingi ya mataifa yote mawili kuheshimiana. Vile vile Javad anaishutumu Uingereza kwa kuiunga mkono Marekani dhidi ya Iran.

Meli ya Uingereza iliyokamatwa na Iran Picha: AFP/N. Kemps

Iran iliikamata meli ya Uingereza kwa madai kwamba ilikataa kujibu mawasiliano ya Iran baada ya kugonga mashua ya uvuvi na zaidi ya kutojibu mawasiliano yao walizima chombo chao cha mawasiliano jambo lililoilazimu kuikamata meli hiyo. Uingereza imakanusha kuzimwa kwa kifaa cha mawasiliano ya meli hiyo na kugongana na chombo chochote na pia meli hiyo ilikuwa katika bahari ya Oman.

Iran inaitaka Uingereze kuiachilia meli yake

Msemaji wa serikali ya Iran amesema jumuiya ya kimataifa inayotaka Iran kuachilia meli ya Uingereza inafaa kutoa ombi hilo pia kwa Uingereza kuachilia meli ya mafuta ya Iran waliyoikamata mapema mwezi huu. Mahakama ya Uingereza iliongeza siku thelathini za kuendelea kuzuiliwa kwa meli hiyo ya Iran kwa jina Grace 1 iliyokamatwa eneo la Gibraltar. Waziri Hunt anasema wanataka kuhakikisha kwamba meli hiyo ilikuwa haipeleki mafuta Syria.

Kuanzia mwezi Mei mwaka huu visa vya meli kushambuliwa vimezidi katika mlango wa bahari wa Hormuz baada ya Umoja wa Mataifa kuongeza idadi ya majeshi kwa kile walichoamini kwamba kuna uwezekano wa vitisho kutoka kwa Iran. Uingereza ilizionya meli zake dhidi ya kutumia njia hiyo ambayo ndiyo njia kuu ya meli za mafuta ya takriban robo tatu ya dunia. 

Serikali ya Uingereza inaulizwa ni kwa nini haikuongeza ulinzi kwa meli zake baada ya tukio la kukamatwa kwa meli ya mafuta ya Irna katika eneo la Gibraltar ambapo bila shaka Iran ilikuwa imekasirishwa na hilo na ilitishia kulipiza kisasi.

(AFPE)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW