Theresa May na Andrea Leadsom kuchuana kuwania nafasi hiyo
8 Julai 2016Ni nani atakuwa Margreth Thatcher mpya? ni habari ambayo iliandikwa katika ukurasa wa mbele wa gazeti la Daily Mail kufuatia Waziri mkongwe katika baraza la Mawaziri nchini humo Theresa May kuongoza kinyan'ganyiro hicho baada ya kupata kura 199 miongoni mwa kura zilizopigwa na wabunge 329 kutoka chama tawala cha Conservative. Waziri mdogo wa nishati wa nchi hiyo Andrea Leadsom ambaye aliingia mara ya kwanza bungeni mnamo mwaka 2010 alipata kura 84.
Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo anatarajiwa kutangazwa Septemba 9, mwaka huu na atakuwa na jukumu la kukamilisha mchakato wa kuiondoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya baada ya kuwa mwanachama kwenye Umoja huo katika kipindi cha miaka 43 kufuatia kura ya maoni iliyofanyika mwezi uliopita.
Theresa May mwenye umri wa miaka 59 anaungwa mkono na wabunge wengi lakini hata hivyo atalazimika kusubiri matokeo ya kura itakayopigwa na wanachama wa kawaida wa chama hicho cha kihafidhina wapatao 150,000 ambao huenda wakahitaji kiongozi ambaye aliuunga mkono Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya wakati wa kura ya maoni.
" Kura hii inaonyesha kuwa chama cha Conservative kitakuwa kimoja na chini ya Uongozi wangu hilo litawezekana" alisema Theresa May.
Kwa upande wake Leadsom ambaye umaarufu wake katika siasa za nchi hiyo ulipanda wakati wa kampeni katika kuelekea kura ya maoni ya kuamua kujitoa au kusalia katika Umoja wa Ulaya na anayetaka nchi hiyo ijiondoe haraka kwenye Umoja huo amepuuza hoja ya uchumi wa nchi hiyo kutetereka endapo itajiondoa kwenye Umoja wa Ulaya akionyesha kuwa na matumaini na hali ya baadaye ya Uingereza hata baada ya kujitoka katika Umoja wa Ulaya.
Mgombea mwingine katika kinyang'anyiro hicho Waziri wa sheria wa nchi hiyo Michael Gove, ambaye alitangaza kuwania nafasi hiyo juma lililopita baada ya awali kuonyesha kumuunga mkono Meya wazamani wa London Boris Johnson aliondolewa katika kinyang'anyiro hicho baada ya kupata kura 46.
Leadsom aungwa mkono na UK Independence Party
Waziri mdogo wa nishati Leadsom tayari anaonekana kuungwa mkono na kiongozi wa chama cha UK Independence Party nchini humo Nigel Farage na Boris Johnson ambaye awali alipewa nafasi kubwa ya kuwa mrithi wa David Cameron katika madaraka hayo ya Waziri Mkuu.
" La muhimu ni kuwa Waziri Mkuu ajaye ni mtu ambaye anaunga mkono Uingereza kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya na ninamuunga mkono" aliandika Farage katika mtandao wa twita baada ya kutangaza Jumatatu wiki hii kuwa alikuwa anastaafu kama kiongozi wa chama cha UK Independence Party.
Theresa May amesema hana mpango wa kutekeleza ibara ya 50 ambayo ni hatua ya mwanzo inayotakiwa kufanywa na nchi inayotaka kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya kabla ya kufikia mwishoni mwa mwaka huu wakati Leadsom amesema angependa kufanya hivyo haraka iwezekanavyo.
Viongozi wa Umoja wa Ulaya wameonya juu ya Uingereza kuchelewesha mchakato wa kujiondoa kwenye Umoja huo hoja ambayo inaungwa mkono pia na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) Christine Lagarde katika mahojiano na Shirika la habari la AFP mjini Washington.
Mwandishi: Isaac Gamba/ AFPE/DPAE
Mhariri: Josephat Charo