1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza kuwa taifa la kwanza kutumia chanjo ya Covid-19

Yusra Buwayhid
2 Desemba 2020

Chanjo iliyotengenezwa kwa ushirikiano kati ya kampuni za Pfizer kutoka Marekani na BioNTech ya Ujerumani, imekuwa ya kwanza kuidhinishwa kutumika dhidi ya ugonjwa wa COVID-19, baada ya kukamilishwa hatua za majaribio.

Biontech Covid-19 Impfstoff
Picha: NurPhoto/picture alliance

Kampuni hizo zimesema mamalaka ya udhibiti wa madawa ya nchini Uingereza imewapa idhini ya matumizi ya dharura ya chanjo hiyo. Kampuni hizo tayari zimeshasaini makubaliano ya kutuma chanko zipatazo milioni 40 nchini Uingereza katika kipindi cha kati ya mwaka 2020 na 2021.

Uingereza ni nchi ya kwanza duniani kuidhinisha chanjo hiyo ya Pfizer/BioNTech ya kupambana na virusi vya corona kwa matumizi ya watu wengi. Mamlaka ya Uingereza ya kudhibiti madawa na bidhaa za afya MHRA, imesema chanjo hiyo ambayo mtu atahitaji kudungwa mara mbili tofauti kila baada ya siku 21, inaweza kutoa ulinzi kwa asilimia 95 dhidi ya ugonjwa wa COVID-19.

Matumizi ya chanjo ya COVID-19 kuanza juma lijalo

Chupa ndogo za mchanganyo wa chanjo ya Covid-19Picha: Laci Perenyi/picture alliance

Na kwamba itaanza kutolewa wiki ijayo. Lakini kwa wale ambao wanaihitaji haraka zaidi, wataanza kupatiwa chanjo hiyo katika siku chache zijazo, mfano watu wanaoishi katika nyumba za kulelea wazee. Uingereza tayari imeshaagiza dozi milioni 40 za chanjo hiyo. Idadi hiyo inategemewa kutosha watu milioni 20. Dozi milioni 10 za chanjo zinatarajiwa kupatikana hivi karibuni, na 800,000 za mwanzo zitafika Uingereza siku chache zijazo. "Wiki ijayo tutapata chanjo 800,000 na huo ni mwanzo tu, kisha tutakuwa tukizitoa kulingana na kasi ualishaji na zinatengezwa na Pfizer nchini Ubelgiji,” ameeleza Matt Hancock, Waziri wa Afya wa Uingereza.

Idhini ya utumiaji wa chanjo hiyo bado inasubiriwa kutolewa katika Umoja wa Ulaya na nchini Marekani, baada ya maombi kuwasilishwa kwa husika mamlaka mapema wiki hii. Mbunge mmoja kutoka Umoja wa Ulaya amesema Uingereza imefanya papara kutoa idhini ya utumiaji wa chanjo hiyo iliyotengenezwa na kampuni za Pfizer na BioNTech. "Nazishauri nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kutorudia uamuzi kama uliofanywa na Uingereza,” amesema leo Peter Liese, mbunge wa Umoja wa Ulaya na mwanachama wa chama cha Kansela wa Ujerumani Angela Merkel.

Hatua ya Uingereza yapongezwa na kampuni Pfizer

Mtendaji mkuu wa Pfizer ameipongeza Uingereza kwa kutoa idhini hiyo ya dharura na kueleza uamuzi huo kuwa ni wa kihistoria katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa COVID-19. Naye mtendaji mkuu wa BioNTech Ugur Sahin amesmea uamzi Uingereza utaisaidia kupunguza idadi ya watu wanaolazwa hospitalini, hasa wale kwenye makundi yaliyo hatarini zaidi ya kupata maambukizi hayo.

Uingereza ni miongoni mwa mataifa yaliyotangaza idadi kubwa ya vifo kutokana na maambukii ya virusi vya corona tangu janga hilo kuanza.

Soma zaidi: Pfizer na BioNTech: Chanjo ya Covid-19 ina ufanisi wa 90%

Zaidi ya watu 60,000 wamepoteza maisha baada ya kupata maambukizi hayo, kulingana na Wizara ya Afya ya Uingereza. Kwengineko ulimwenguni, katika nchi kama Urusi, China na Bahrain, chanjo dhidi ya virusi vya corona zimeshaanza kutumika. Hata hivyo, bado haijulikani hakika zina ufanisi wa kiasi gani na iwapo zina madhara yoyotekwa afya ya binadamu.

Vyanzo: dpa,rtre,afp

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW