Uingereza: Manchester United yamfuta kazi Jose Mourinho
18 Desemba 2018Mechi ya mwisho ya kocha huyo ambaye ni raia wa Ureno ilikuwa na viongozi wa ligi hiyo, Liverpool siku ya Jumapili ambapo Manchester walifungwa mabao matatu kwa moja. Kufutwa kazi kwa Mourinho kunajiri miaka miwili unusu tangu alipojiunga na klabu hiyo, na miaka mitatu na siku moja baada ya klabu ya Chelsea kumfuta kazi, miezi kadhaa baada ya kuwaongoza kutwaa kombe la ligi hiyo.
Vile vile inajiri wakati ambapo kumekuwepo msuguano kati yake na Paul Pogba, ambaye mara nyingi amekuwa hachezeshwi katika kikosi cha kuanza mechi. Baada ya taarifa hiyo kutolewa, Pogba aliandika ujumbe ulioonekana kuwa wa kejeli kwenye Twitter lakini baada ya muda mfupi akaufuta. Aliyekuwa mchezaji wa timu hiyo, Michael arrick ambaye ni mmoja wa walio katika safu ya kiufundi, anatarajiwa kushikilia nafasi ya Mourinho kikaimu, lakini United imesema kwamba kocha wa muda atateuliwa kuhudumu hadi mwishoni mwa msimu.
Licha ya timu hiyo kufika awamu ya mchujo katika ligi ya UEFA, wanakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa klabu ya Paris Saint German..mkusanyiko wa matokeo, tofauti zilizoibuka na ukosoaji wa sera ya uhamisho ya bodi ya United zimethibitisha kuwa masuala yaliyochangia kufutwa kwa Mourinho.
Kulingana na vyombo vya habari vya Uingereza, Manchester United itamlipa Mourinho Dola milioni 28 kwani bado klabu hiyo iko kwenye ligi ya UEFA. Wanaopigiwa upatu kuchukua nafasi ya Mourinho ni aliyekuwa kocha wa Real Madrid Zinedine Zidane na wa Tottehnham Hotspur Mauricio Pochettino.
Kwa sasa Manchester United ni nambari sita katika ligi ya Premier kwa alama 26 baada ya kucheza mechi 17, alama 19 nyuma ya viongozi Liverpool. Mourinho alishinda Ligi ya Europa na Kombe la Ligi msimu wa mwaka 2016-2017, kabla ya kuiongoza United hadi nafasi ya pili katika ligi hiyo msimu uliopita na kufika fainali ya Kombe la FA.
Mwandishi: Sophia Chinyezi/AFPE/DPAE
Mhariri: Josephat Charo