Muda wa mwisho wa uhamishaji Afghanistan ni mwisho wa mwezi
25 Agosti 2021
Waziri Raab ameliambia shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC kwamba wanafikiria kuwa zoezi hilo litaendelea hadi mwisho wa mwezi Agosti lakini wapangaji wa kijeshi watathibitisha maelezo ya muda sahihi wa kufanya hivyo na kuongeza kuwa Uingereza inatarajia kuwepo kwa uwanja wa ndege unaoendesha shughuli zake mjini Kabul baada ya kumalizika kwa zoezi hilo la uhamishaji.
Raab pia amesema kwamba Inaonekana wazi kwamba vikosi vya kijeshi vya kigeni vitaondolewa kufikia mwisho wa mwezi na kwamba kile watakachokifanya ni kutumia kila saa na siku iliyobakia kuwaondoa raia wao kama watakavyoweza, Waafghanistan waliowafanyia kazi na tayari wamewaondoa wanahabari, watetezi wa haki za wanawake na wasomi walio chini ya msaada wa masomo wa Uingereza(Chevening).
Raab ameongeza kuwa, iwapo uongozi wa Taliban utataka uwanja wa ndege unaofanya kazi, uchumi unaofanya kazi hata katika kiwango cha kawaida, itaubidi kurekebisha mienendo yake kuhusu jinsi unavyofanya shughuli zake na hivyo itaamanisha kwamba utapaswa kuzingatia ujumuishaji na pia kutoa hakikisho kwa watu nchini humo na pia kwa washirika wa kimataifa ambao utabidi kuwategemea.
Wakati huohuo, video zilizochapishwa katika mitandao ya kijamii zimeonesha maelfu ya watu wakiwa bado wamekusanyika katika maeneo ya uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kabul hii leo asubuhi kwa matumaini ya kupata ndege ya kuwahamisha kutoka Afghanistan. Picha za video hizo zimeonesha mamia ya Waafghanistan wakisubiri kwenye mahandaki nje ya uwanja wa ndege wengine wakisimama ndani ya maji yaliowafikia viunoni. Nchi zimeanza kuwachukuwa raia wao kutoka maeneo mengine na kuwaleta ndani ya uwanja huo wa ndege kutokana na hali ya machafuko katika milango ya uwanja huo wa ndege.
Huku hayo yakijiri, katika ujumbe aliouandika katika ukurasa wake wa twitter, mmiliki wa shule moja ya binafsi nchini Afghanistan, Shabana Basij-Rasikh amesema wanafunzi wa shule hiyo wapatao 250, walimu wao na familia zao wako njiani kwenda katika taifa la Rwanda kupitia Qatar na kwamba wanakusudia kuanza muhula mwingine wa masomo nje ya nchi kwa wanafunzi wao wote. Basij-Rasikh amesema kuwa wakati hali itakapokuwa shwari, wanatarajia kurudi nyumbani nchini Afghanistan.
Mjini Kigali, msemaji wa serikali ya Rwanda Yolande Makolo amethibitisha habari hizo. Makolo ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba wanaikaribisha jamii hiyo ya SOLA nchini Rwanda na kwamba wanaheshimu ombi lao la faragha kwa hivyo hakutakuwa na maelezo zaidi. Siku chache mapema, Basij-Rasikh alisema kuwa anateketeza rekodi zote za masomo za wanafunzi wake katika juhudi za kuwalinda na familia zao.