1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUingereza

Uingereza na EU zafikia mkataba wa baada ya Brexit

27 Februari 2023

Uingereza na Umoja wa Ulaya zimefikia makubaliano juu ya kanuni za biashara za baada ya Brexit zitakazotumika huko Ireland Kaskazini.

England Brexit Rishi Sunak und Ursula von der Leyen
Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak (kulia) akiwa pamoja na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen.Picha: Steve Reigate/empics/picture alliance

Iwapo mkataba huo utaridhiwa na wanasiasa wa Ireland Kaskazini itakuwa hatua muhimu ya kusawazisha msuguano mkubwa uliokuwepo kati ya Brussels na serikali mjini London tangu Uingereza ilipojitoa rasmi kutoka Umoja wa Ulaya mwaka 2020. 

Taarifa kuhusu kupatikana kwa mkataba huo zimetolewa jioni ya Jumatatu baada ya mazungumzo kati ya waziri mkuu wa Uingereza Rishi Sunak na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen.

Bibi Von der Leyen alikwenda mjini London akiwa na ajenda moja kubwa nayo ni kufanikisha kupatikana mkataba huo. Taarifa za kupatikana mkataba huo zimetolewa na Shirika la Habari la Uingereza BBC.

Sunak na Von der Leyen walikuwa wamepangiwa kuzungumza na waandishi habari kufafanua vipengele vya mkataba uliopatikana.

Je, makubaliano hayo yatamaliza mvutano kati ya Uingereza na Umoja wa Ulaya?

Picha: Dan Kitwood/AP/picture alliance

Kupatikana makubaliano hayo kunahitimisha mwaka mzima wa majadiliano juu kile kinachofahamika kama "Itifaki ya Ireland Kaskazini".

Itifaki hiyo iliridhiwa mwaka 2020 kama sehemu ya mkataba wa Uingereza kujitoa rasmi kutoka Umoja wa Ulaya. Itifaki hiyo ililiacha eneo la Ireland Kaskazini ambalo ni sehemu ya Uingereza chini ya kanuni za biashara zinazoongoza soko huria la Umoja wa Ulaya.

Hiyo ilimaanisha licha ya Uingereza kutokuwa tena sehemu ya Umoja wa Ulaya, sehemu ya ardhi yake bado ililazimika tangu wakati huo kutii masharti ya biashara ya Umoja wa Ulaya.

Hali hiyo ililazimisha kuwepo kwa ukaguzi mkali wa bidhaa zinatoka maeneo mengine ya Uingereza na kwenda kuuzwa Ireland Kaskazini.

Sababu za kuwepo itifaki ya Ireland Kaskazini ilikuwa ni kuzuia kuwepo mtafaruku kwenye mpaka kati ya Ireland Kaskazini ambayo ni sehemu ya dola ya Uingereza na jirani yake Jamhuri ya Ireland, ambayo ni taifa huru na mwanachama wa Umoja wa Ulaya.

Wakati pande zote mbili yaani Uingereza na Jamhuri ya Ireland zilipokuwa wanachama wa Umoja wa Ulaya, usafirishaji wa bidhaa na shughuli nyingine za biashara zilikuwa zikifanyika bila vizuizizi vya mpakani.

Hata hivyo mchakato wa Brexit ulibadili kila kitu na kwa malengo ya kuepeusha ukaguzi kwenye mpaka baina ya Ireland mbili ilikubaliwa Ireland Kakszaini ibakie chini ya kanuni za biashara za Umoja wa Ulaya.

Mtafaruku ulilazimisha kufanyika mazungumzo ya kutafuta mkataba mpya

Picha: Federico Gambarini/dpa/picture-alliance

Tangu baada ya Brexit mwaka 2020, serikali ya Uingereza imekabiliwa na shinikizo la ndani la kutaka Itifaki ya Ireland Kaskazini ifutwe au kupatikane mkataba mwingine utakaosawazisha kanuni za biashara.

Wakati fulani viongozi mjini London walitishia kuchukua uamuzi wa upande mmoja wa kufutilia mbali itikafi ya Ireland Kaskazini jambo lilizitumbukiza Uingereza na Umoja wa Ulaya kwenye msuguano wa kidiplomasia.

Hatua ya kupatikana mkataba mpya inatarajiwa itamaliza tofauti zilizopo. Hata hivyo mkataba huo utapaswa kuungwa mkono na wanasiasa wa chama cha Democratic Unionist, DUP, cha Ireland Kaskazini ambao walikuwa wakiipinga kabisa itikafi ya baada ya Brexit.

Mkuu wa chama hicho Jeffrey Donaldson amesema chama chake kitahitaji muda kuungalia kwa karibu mkataba uliopatikana.

Akizungumza na BBC Donaldson amesema "Siwezi kusema ninaunga mkono au ninapinga, tunahitaji muda kutizama kile kilichomo na ni vipi kinarandana na vigezo vyetu saba" 

Chama hicho kinachopigania muungano thabiti wa Uingereza kinadai kanuni za itifaki iliyokuwepo zimeikuwa zikitishia nafasi ya Ireland Kaskazini ndani ya dola ya Uingereza.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW