1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza na Iran zafungua balozi zao

23 Agosti 2015

Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza Philip Hammond amesema atafungua tena ubalozi wa nchi hiyo nchini Iran leo Jumapili(23.08.2015), miaka minne tangu ubalozi huo uliposhambuliwa.

Iran Teheran Britische Botschaft
Ubalozi wa Uingereza mjini TehranPicha: picture-alliance/dpa/A. Taherkenareh

Ubalozi huo ulishambuliwa na kuharibiwa na kundi la watu, na wakati huu hali ya mahusiano na Tehran inaanza kuwa mazuri tena na mataifa ya magharibi.

Ubalozi wa Iran mjini London utafunguliwa pia katika wakati huo huo, Hammond amesema, mwanzoni kwa kiwango cha afisa mkuu wa ubalozi, kwa mtazamo wa kuwarejesha mabalozi wa nchi hizo mbili katika miezi michache ijayo.

Ubalozi wa Uingereza mjini Tehran uliwa umevamiwa na wanafunziPicha: dapd

Maafisa wa bara la Ulaya wamekuwa wakifanya ziara za haraka mjini Tehran tangu Julai 14 , wakati Iran ilipofikia makubaliano na Uingereza, China, Ufaransa, Ujerumani , Urusi na Marekani , na yaliyomaliza mkwamo wa miaka 13 kuhusiana na mpango wa nyuklia wa Iran.

Hatua ya pili itashuhudia kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa dhidi ya Iran na kuzusha wimbi la shauku kutoka kwa nchi zinazotaka kurejesha tena uhusiano na jamhuri hiyo ya Kiislamu yenye utajiri wa mafuta.

Hammond yuko mjini Tehran

Ziara ya Hammond ni ya kwanza kufanywa na waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza tangu mwaka 2003.

Wanafunzi wakifanya uharibifu katika ubalozi wa Uingereza mjini Tehran Novemba 29 , 2011Picha: dapd

"Miaka minne hadi sasa kutoka wakati wa shambulio dhidi ya ubalozi wa Uingereza, leo naufungua tena, " Hammond amesema katika taarifa.

"Wairani wakati huo huo watafungua ubalozi wao mjini London. Uhusiano wetu umekuwa bora tangu mwaka 2011."

Hali hiyo ilianzia Juni mwaka 2013 wakati alipochaguliwa rais wa sasa wa Iran Hassan Rouhani , mtu anayesifiwa kuwa mwenye siasa za wastani ambaye ameyanyoonyeshea mkono mataifa ya magharibi.

"Kuchaguliwa kwa rais Rouhani pamoja na makubaliano ya mwezi uliopita ni matukio muhimu. Naamini kwamba tuna uwezo wa kwenda mbali zaidi," amesema Hammond.

Wanafunzi wakiandamana kupinga vikwazo vilivyoongozwa na UingerezaPicha: dapd

Kufuatia shambulio la mwaka 2011 katika ubalozi, Uingereza ilisema haingewezekana kutokea bila ya ridhaa kamili ya uongozi wa Iran katika wakati huo.

Hali hiyo ilitokea baada ya bunge la Iran kupiga kura kumfukuza balozi wa Uingereza na kupunguza uhusiano wa kibiashara na Uingereza kwa ajili ya vikwazo vilivyoongozwa na Uingereza dhidi ya sekta ya mabenki ya Iran.

Wanafunzi wafanya vurugu

Wanafunzi walifanya vurugu na uharibifu mkubwa kwa saa kadhaa katika viwanja vya ubalozi huo wa Uingereza mjini Tehran , wakichana bendera ya Uingereza, wakiharibu picha ya malkia Elizabeth wa pili na kuzivuruga ofisi.

Wafanyakazi walikamatwa na waandamanaji. Uhusiano wa kibalozi ulipunguzwa kwa kiwango cha chini kabisa kadri ilivyowezekana, wakati Uingereza ikiwafukuza maafisa wa Iran.

"Kufunguliwa kwa balozi ni hatua muhimu ya kuimarisha uhusiano kati ya nchi zetu," amesema Hammond. "katika hatua ya kwanza, tutataka kuhakikisha kwamba makubaliano ya nyuklia yanafanikiwa, ikiwa ni pamoja na kuhimiza biashara na uwekezaji mara baada ya vikwazo kuondolewa."

Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza Philip HammondPicha: Getty Images/AFP/D. Hill

Amesema Uingereza na Iran zinapaswa pia kuwa tayari kujadiliana kuhusu changamoto ikiwa ni pamoja na ugaidi,uthabiti wa kikanda, na kusambaa kwa kundi la kijihadi la Dola la Kiislamu nchini Syria na Iraq.

"Hatua hiyo haina maana kwamba tunakubaliana katika kila kitu. Lakini ni sahihi kwamba Uingereza na Iran zinapaswa kuwa na uwakilishi katika kila nchi, amesema Hammond.

Mipango hiyo ya kuzifungua balozi hizo ilitangazwa Juni mwaka jana.

Mwandishi : Sekione Kitojo / afp

Mhariri:

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW