Viongozi wa Uingereza na Ufaransa wakutana
18 Januari 2018Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May amemkaribisha rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anayefanya safari yake ya kwanza rasmi nchini Uingereza, akitumia njia ya bahari inayozitenganisha Ufaransa na Uingereza hadi kwenye kambi ya kijeshi iliyo karibu na jiji la London.
Viongozi hao wanatarajiwa kujadili masuala ya usalama, uhamiaji, sera za nje, biashara na uhusiano wa nchi hizo mbili. Kukutana kwa viongozi hao ni sehemu ya kujenga uhusiano wao wakati ambapo Uingereza inajiandaa kuondoka kutoka kwenye Umoja wa Ulaya.
Bi Theresa May anatarajiwa kutangaza kuwa nchi yake itaipa Ufaransa kiasi cha pauni milioni 45 kwa ajili ya kuisaidia kupambana na uhamiaji haramu katika miji ya pwani pamoja na kwenye njia ya bahari inayozitenganisha Ungereza na Ufaransa.
Msemaji wa serikali ya Uingereza kutoka makao ya waziri mkuu ya Downing Street amesema fedha hizo zitatumika kwa kujenga uzio na kufunga kamera za video zenye teknolojia ya ufuatiliaji na ugunduzi katika eneo la Calais na kwenye bandari za karibu za nchini Ufaransa.
Pia fedha hizo zitasaidia katika shughuli za kuwahamisha wakimbizi kwa ajili ya kuzuia kuchipuka kwa kambi nyingine ya wakimbizi.
Siku mbili zilizopita kabla ya rais wa Ufaransa kuanza safari yake alizuru kambi ya Calais na alisema nchi yake haitaruhusu kamwe kurejea kuchipuka kwa kambi hiyo. Macron amesema kila mmoja wetu anapaswa kufahamu kwamba zitafanyika kila aina ya jitihada kuhakikisha kwamba safari zilizo kinyume cha sheria kuelekea nchini Uingereza haziwezekani.
Rais wa Ufaransa amesema Calais sio mlango wa kuingilia Uingereza na kwamba makundi yanayofanya biashara haramu ya kuwasafirisha hayapewi nafasi.
Bibi May na rais wa Ufaransa walijumuika pamoja kwenye dhifa ya chakula cha mchana katika eneo bunge la Theresa May la Maidenhead, magharibi mwa London, na kisha kuandamana pamoja hadi eneo lililo karibu la Sandhurst kwenye chuo cha kijeshi cha Royal Military Academy kwa ajili ya kuhudhuria mkutano huo mkuu.
Namna ya kukabiliana na maelfu ya wahamiaji hasa kutoka Mashariki ya Kati na mataifa ya Kiafrika limekuwa ni suala lenye changamoto nyingi kwa nchi hizi mbili kwa miaka kadhaa,hasa baada ya kuchipuka kambi ya wakimbizi ya Calais nchini Ufaransa.
Hatua za kuboresha usalama mnamo mwaka 2015 na kufungwa kwa eneo kuu la kambi hiyo mnamo mwaka 2016 zilisaidia kupunguza visa vya watu waliojaribu kuingia Uingereza kinyume cha sheria kutoka watu zaidi ya elfu 80 mnamo mwaka 2015 hadi watu elfu 30 kufikia mwaka jana.
Vyanzo vya mjini Paris vilisema kwamba Theresa May na Emmanuel Macron wanatarajiwa pia kutangaza aina mpya ya ushirikiano baina ya nchi hizi mbili ambayo yanasisitiza makubaliano ya Le Touquet, makubaliano hayo yanahusu udhibiti wa mipaka katika njia ya bahari inayozitenganisha nchi hizo katika eneo la kaskazini-magharibi mwa Ufaransa na kusini mashariki mwa Uingereza.
Mwandishi: Zainab Aziz/DPAE/AFPE
Mhariri: Gakuba Daniel