Uingereza na Ujerumani kuimarisha ushirikiano wa ulinzi
23 Oktoba 2024Mpango huo unajumuisha ahadi ya kutengeneza silaha mpya za masafa marefu. Washirika hao wawili wa NATO wamesema muafaka huo, unaofahamika kama Trinity House Agreement, utaimarisha uwezo wao wa kushirikiana na kufanya luteka za kijeshi kwenye mpaka wa mashariki mwa jumuiya hiyo, na kuboresha uwezo wao wa kuzuia mashambulizi kutokana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Akizungumza mjini London, Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius amesema makubaliano hayo yatasaidia katika miradi ya ulinzi wa angani, ardhini, baharini na mitandaoni. Waziri wa Ulinzi wa Uingereza John Healey amesema Ujerumani mara kwa mara itaziweka ndege zake nchini Scotland kusaidia kulinda Bahari ya Atlantiki ya kaskazini. Aidha, kampuni kubwa ya kutengeneza silaha ya Ujerumani - Rheinmetall itafungua kiwanda kipya kitakachounda nafasi za kazi 400 na kuwa mtengenezaji wa kwanza wa mizinga ya kivita nchini Uingereza kwa muongo mmoja.