Uingereza na Ulaya zaiwekea Urusi vikwazo zaidi
20 Mei 2025
Uingereza na Ulaya zimesema vikwazo vyao vitalenga meli 18 zinazobeba mafuta ya Urusi pamoja na kampuni za fedha zilizowasaidia kukwepa athari ya vikwazo vya awali ilivyowekewa kutokana na hatua yake ya kujiingiza na kuanzisha vita nchini Ukraine.
Uingereza imesema vikwazo hivyo pia vitalenga sekta za kijeshi na usafirishaji wa nishati muhimu. Vitalenga mtandao wa usambazaji silaha ikiwemo mabomu ya Iskander ambayo yamekuwa yakivurumishwa katika maeneo ya watu wakati wa vita. Imesema Putin amekuwa akiyatumia mabomu hayo bila kujali maisha ya watu, huku akitolea mfano shambulio dhidi ya Sumy lililofanyika mwezi Aprili ambalo Ukraine ilisema liliwaua watu 34 wakiwemo watoto.
Ulaya yataka hatua kali zichukuliwe na Marekani dhidi ya Urusi kama makubaliano hayatofikiwa
Akiandika katika ukurasa wake wa Telegram, baada ya vikwazo hivyo vipya, rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy aliwashukuru wote wanaoendelea kuwawekea vikwazo waanzilishi wa vita.
"Vikwazo ni muhimu, nawashukuru wote wanaovifanya kuwa na nguvu kwa watu wanaoanzisha vita," alisema rais Zelensky.
Vikwazo hivyo pia vitawalenga wanachama 14 wa taasisi ya SDA inayotoa taarifa za operesheni zinazodaiwa kuhujumu uhuru, demokrasia na utawala wa sheria wa Ukraine na dunia nzima. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uingereza David Lammy amesema mashambulizi anayoyafanya putin nchini Ukraine yanaonyesha wazi kwamba nikiongozi anaependa vita.
Marekani inashinikzwa kutoiruhusu Urusi kuendelea na vita Ukraine
Kwa upande wake Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Johann Wadephul, amesema Ujerumani imekuwa wazi kabisa kwamba kile inachohitaji kutoka Urusi ni usitishwaji wa mapigano bila masharti. Amesema hadi sasa Urusi haijakubali hilo na ndio maana imewekewa vikwazo. Ujerumani imesema inatarajia Marekani ambae ni mshirika wa Ulaya kutoruhusu Urusi kuendelea na vita vyake nchini Ukraine.
Hata hivyo Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Urusi kupitia msemaji wake Maria Zakharova imesema Urusi haitishiki.
Zelensky akutana na viongozi wa Marekani, EU mjini Rome kabla ya simu ya Trump na Putin
Ulaya imekuwa ikiushinikiza utawala wa Marekani kuiunga mkono katika kuiwekea Urusi vikwazo. Viongozi wa Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Polanda kwa pamoja walisafiri mjini Kiev mapema mwezi huu na walionekana wakizungumza na Trump pamoja na Zelensky. Kwa upande wake Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas amesema vikwazo vingine vinafanyiwa kazi na wanaisubiri Marekani kuchukua hatua.
Wakati huo huo Mawaziri wa mambo ya kigeni wa nchi tajiri kiviwanda duniani za kundi la G7 wanakutana nchini Canada na kando na kujadili uchumi wa dunia na hatua ya ushuru unaowekwa na Trumo pamoja na vita vya kibiashara pia wanajadili kuhusu vita vya Urusi na Ukraine.
afp/ap/reuters