Uingereza na Ureno kulitambua taifa la Palestina Jumapili
21 Septemba 2025
Uingereza na Ureno zinatarajiwa hii leo kulitambua taifa la Palestina, kabla ya mkutano muhimu wa Umoja wa Mataifa ambapo nchi mbalimbali zinatazamiwa pia kuchukua mwelekeo kama huo ili kuzidisha shinikizo kwa Israel kuhusu vita vya Gaza. Takribani mataifa 10 yanatarajiwa kulitambua rasmi taifa la Palestina katika siku zinazokuja, huku ripoti za vyombo vya habari vya Uingereza ikiwemo BBC vikiripoti kwamba Waziri Mkuu Keir Starmer atatangaza mwelekeo mpya wa kisera leo Jumapili wakati Israel ikipinga vikali. Idadi kubwa ya washirika wa muda mrefu wa Israel, wamebadili msimamo wao katika miezi ya hivi karibuni, wakati Israel ikizidisha mashambulizi yake dhidi ya Gaza yaliyochochewa na shambulio la wanamgambo wa Hamas mwaka 2023. Eneo la Wapalestina lililozingirwa limeharibiwa vibaya, vifo vingi na ukosefu mkubwa wa chakula ambao umesababisha janga kubwa la kibinadamu.