Uingereza yaandaa mapokezi makubwa kwa Trump
16 Septemba 2025
Ratiba ya mapokezi ilionesha ulinzi mkali tangu kuwasili kwake mpaka kuhudhuria kwenye tafrija ya chakula cha jioni akiwa ameandamana na Mfalme Charles wa Tatu, lakini ni wazi kuwa upinzani dhidi ya Trump, mwenye umri wa miaka 79 na ambaye mama yake ametokea Scotland, utajitokeza hata kabla ya ziara hiyo.
Maelfu ya watu walitarajiwa kujipanga kwenye njia ambazo msafara wa Trump na Mfalme Charles ungelipita wakipaza sauti na kuonesha mabango ya kupinga siasa za Trump ulimwenguni.
Polisi ya Thames Valley ilisema imetuma kikosi chake maalum kuzunguka Kasri la Windsor anakofikia Trump kama sehemu ya hatua pana za kiusalama, na kwamba kikosi hicho kinajumuisha askari wa kawaida na askari kanzu.
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza, Downing Street, ilisema kwenye taarifa yake kwamba ziara hiyo ya Trump ingelithibitisha jinsi urafiki usioyumba baina ya nchi hizo mbili ulivyofikia viwango vya juu kabisa.
Mikataba ya mabilioni
Pande hizo mbili zilitazamiwa kusaini msururu wa mikataba yenye thamani ya hadi paundi bilioni 10, ukiwemo ule wa kuharakisha miradi ya nyuklia na pia ule maafisa wa Uingereza wanaouita "ubia wa teknolojia unaongoza duniani".
Kuelekea ziara hiyo ya Jumanne (Septemba 16), tayari kampuni ya Google ilishasema kwamba ingeliwekeza kiasi cha paundi bilioni 5 nchini Uingereza ndani ya kipindi cha miaka miwili ijayo, huku kampuni nyengine za Marekani, zikiwemo za PayPal na Citi Group, zikitangaza uwekezaji wa paundi bilioni 1.25.
Mbali na utiaji saini mikataba hiyo, suala la vita vya Urusi nchini Ukraine lilitazamiwa kuchukuwa nafasi kubwa ya mazungumzo kati ya Trump na Waziri Mkuu wa Uingereza , Keir Starmer.
Starmer ni miongoni mwa viongozi wa Ulaya ambao wamekuwa wakimshinikiza Trump kuendelea kuiunga mkono Kiev, wakihofia kwamba kiongozi huyo wa Marekani anaelemea zaidi upande wa Rais Vladimir Putin wa Urusi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, alisema siku ya Jumanne kwamba kulikuwa na uwezekano Trump kukutana na Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine wiki ijayo na kwamba bado alikuwa na matumaini ya kufanikisha makubaliano ya amani kati ya Kiev na Moscow.
Kwa upande wake, mke wa Trump, Melania, ambaye anaambatana na mumewe kwenye ziara hii, alionekana kuwa na ratiba tafauti.
Alitazamiwa kushirikiana na Malkia Camilla, ambaye anaendelea kupana ahuweni baada ya kusumbuliwa na maradhi yaliyomfanya ashindwe kuhudhuria mazishi ya mtawala wa Kent siku ya Jumanne.