Ulaya yasema haitotetereka
24 Juni 2016"Ni kipindi cha kihistoria lakini bila ya shaka halibidi kuwa jambo la pupa" amesema mwenyekiti wa baraza la ulaya Donald Tusk aliyezungumza kwa niaba ya mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya,lengo likiwa kuhakikisha radi ya London haitaidhuru Brussels."Si siri kuwa tulitaraji matokeo ya kura ya maoni yangekuwa ya aina tofauti. Nnatambua fika kishindo cha kisiasa kilichojitokeza wakati huu. Nnataka kumhakikishia kila mmoja tumejiandaa kukabiliana na hali kama hii isiyo ya kuridhisha."Amesema mwenyekiti wa baraza la ulaya Donald Tusk.
Umoja wa ulaya hautasambaratika
Mwenyekiti wa baraza la Ulaya amesema wamepania kuendelea na muungano wa mataifa 27 na kuhakikisha hakutakuwa na mwanya wa kisheria hadi Uingereza itakapojiondowa rasmi katika Umoja wa ulaya.
Mfululizo wa madhara utakaochochewa na wale wanaoupinga Umoja wa Ulaya hautatokea amesema spika wa bunge la Ulaya Martin Schulz kupitia kituo cha pili cha televisheni ya Ujerumani ZDF.
Hata hivyo viongozi wa makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia hawajakawia kuyatumia matokeo ya kura ya maoni ya Uingereza,mfano wa mwenyekiti wa chama cha Front National cha Ufaransa Marine Le Pen,mbunge wa Uholanzi Geert Wilders na Matteo Salvini wa Italy waliotoa wito wa kuitishwa kura kama hiyo ya maoni nchini mwao.
Martin Schulz anasema atakutana hivi punde na kansela Angela Merkel wa Ujerumani kuzungumzia namna ya kuepusha balaa la kusambaa hisia dhidi ya Umoja wa Ulaya. Mapema leo asubuhi Martin Schulz alizungumza kwa simu na mwenyekiti wa baraza la Ulaya Donald Tusk na mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker.
Kura ya Brexit ni chachu ya kuufanyia mageuzi Umoja wa Ulaya
Waziri mkuu wa Uholanzi Mark Rutte ambae nchi yake ndio mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Ulaya ameitisha pia mkutano wa maafisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels. Mark Rutte anasema uamuzi wa Uingereza umemvunja moyo hata hivyo anasema unabidi uwe chachu ya kuufanyia marekebisho Umoja huo.
Wakati huo huo mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa mataifa sita waasisi wa Umoja wa Ulaya watakutana Berlin kesho kutathmini madhara ya kura ya Brexit-hayo yametangazwa na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Franck Walter Steinemeier aliyeitaja siku ya leo kuwa ni siku ya huzuni kwa Uingereza na Umoja wa ulaya.
Nae rais Francois Hollande wa Ufaransa amepanga kutoa taarifa yake kuhusiana na kujitoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya baadae hii leo.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP
Mhariri:Yusuf Saumu