1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza yaihusisha Urusi na tukio la kupewa sumu Jasusi

Isaac Gamba
13 Machi 2018

Uingereza itakuwa na kikao cha dharula leo kuhusiana na tukio la kupewa sumu jasusi wa zamani wa Urusi katika ardhi ya Uingereza baada ya Marekani na Jumuiya ya kujihami ya NATO kuunga mkono madai hayo ya Uingereza.

England Theresa May Salisbury incident
Picha: picture-alliance/dpa/empics/PA Wire

.Wakati mgogoro huo wa kidiplomasia ukipamba moto, Urusi imekanusha madai ya kuhusishwa na shambulizi hilo dhidi ya Sergei Skripal pamoja na binti yake Yulia, kusini magharibi mwa Uingereza mnamo Machi 4.

Skripal afisa wa zamani wa kijasusi aliyewahi kufungwa jela kwa kuuza siri za Urusi kwa Uingereza, alihamia Uingereza mwaka 2010 na kuishi katika mji waSalsbury nchini humo.

Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May amelieleza bunge kuwa inaelekea kwa kiwango kikubwa Urusi iko nyuma ya tukio hilo na kuipa Urusi hadi mwishoni mwa Jumanne kujibu tuhuma hizo matamshi ambayo yanazusha uvumi kuwa Uingereza huenda ikatoa mwito kwa washirika wake kuiunga mkono.

Marekani na NATO zote zilitoa taarifa kuiunga mkono Uingereza wakati wasiwasi ukiongezeka kutokana na matumizi ya kile May alichoeleza matumizi ya silaha ya sumu iliyotengenezwa Urusi.

Skripal, 66, na binti yake Yulia mwenye umri wa miaka 33 wako bado hospitali katika hali mbaya baada ya kukutwa wakiwa hawajitambui katika viti nje ya mtaa wenye maduka katika mji wa Salisbury nchini Uingereza.

Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Reuters/M. Shemetov

Wafanyakazi wa idara ya dharula wametawanywa katika maeneo ya mji huo huku kiasi ya watu 500 wanaoweza kuwa wameathiriwa na sumu hiyo wametakiwa kufua nguo zao na pamoja na vitu vingine vinavyowahusu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, RexTillerson amewaeleza waandishi wa habari kuwa ana imani na uchunguzi  unaofanywa na Uingereza na kusisitiza kuwa wale wote waliofanya uhalifu huo na wale walioagiza lazima wachukuliwe hatua kali za kisheria.

Akilihutubia bunge la nchi hiyo,  May amesema ni wazi sasa kuwa Skripal na binti yake wamedhurika na aina ya sumu iliyotengenezwa na kulingana na uchunguzi uliofanywa na wataalamu waliobobea katika masuala ya kisayansi na ulinzi na kwa kuzingatua kuwa Urusi imewahi kutengeneza sumu ya aina hiyo anathibitisha kuwa Urusi na bado itaendelea kufanya hivyo.

Uingereza yaitaka Urusi kutoa maelezo bayana 

May ameongeza kusema kuwa Uingereza imeipa Urusi hadi leo mwisho wa kueleza bayana juu ya taarifa zinazohusiana na maendeleo ya mpango wa sumu hiyo katika shirika linalozuia matumizi ya silaha za sumu.

Ameonya kuwa iwapo hakutakuwa na maelezo ya kutosha basi itahitimisha kuwa tukio hilo ni matumizi ya nguvu kinyume cha sheria yaliyofanywa na serikali ya Urusi dhidi ya Uingereza na kuonya kuchukua hatua zote zinazostahiki.

Gazeti la Daily Telegraph la nchini Uingereza limeripoti leo kuwa Uingereza ilikuwa inashauriana na washirika wake wa NATO juu ya uwezekano wa kutumia ibara ya tano inayohusiana na ushirikiano wa pamoja katika masuala ya ulinzi.

Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg amesema tukio hilo linazua wasiwasi mkubwa na kuwa NATO kwa sasa inafanya mawasiliano na maafisa wa Uingereza kuhusu suala hilo.

Alipozungumza na shirika la utangazaji la Uingereza, BBC, Rais wa Urusi, Vladimir Putin amepuuza madai ya Urusi kuhusishwa na shambulizi hilo la sumu inayopunguza kasi ya mapigo ya moyo na wakati mwingine kusababisha kifo.

Mapema jana Urusi iliyakataa matamshi hayo ya May na kusema ni jaribio la kuvuruga imani dhidi ya Urusi ambayo ni mwenyeji wa fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia.

Mwandishi: Isaac Gamba/AFPE

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW