Uingereza yaimarisha vizuizi kukabiliana na Omicron
9 Desemba 2021Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amesema hatua hizo zinakusudia kuzuia wimbi la wagonjwa hospitalini na vifo, wakati kirusi cha Omicron kikisambaa kwa kasi nchini humo. Johnson ameongeza kwamba visa vya Omicron vinaongezeka mara mbili kila baada ya siku mbili hadi tatu. Hadi kufikia sasa Uingereza imerekodi visa 568 vya kirusi cha Omicron.
"Bado hatujui ukali wa Omicron, kiwango chake halisi cha maambukizi, wala ufanisi kamili wa chanjo zetu dhidi yake. Ni jambo la uwajibikaji kuhamia mpango B nchini Uingereza. Kwa hivyo tunapunguza kasi ya kuenea kwa virusi, ili tupate muda zaidi wa kudungwa chanjo ya nyongeza na haswa kwa wazee na walio hatarini zaidi, na kuelewa majibu ya maswali muhimu kuhusu Omicron."
COVID: Je kirusi cha omicron ni hatari kiasi gani?Aidha Waziri Mkuu Johnson ameongeza kwamba kirusi cha Omicron kinasambaa kwa haraka zaidi kuliko kirusi kilichopita cha Delta. Vizuizi hivyo havitofunga shughuli nchini humo na badala yake watu wataendelea na hafla za Krismasi kama kawaida lakini wakilazimika kuonyesha cheti cha chajo kwa mara ya kwanza. Wanasayansi katika shirika la usalama la afya la Uingereza wamesema wanatarajia kirusi cha Omicron kitashika makali nchini humo ndani ya wiki mbili hadi nne zijazo.
Hatua hizo zimetangazwa wakati waziri mkuu Johnson na serikali yake wakikabiliwa na ongezeko la shinikizo juu ya ripoti za msaidizi wake mmoja kukiuka kanuni za Covid-19 wakati nchi ilipofungwa mwaka jana.
Wakati huo huo kampuni kubwa ya dawa ya Pfizer na mshirika wake BioNTech zimetangaza kwamba dozi ya tatu ya chanjo yao dhidi ya Covid-19, inatoa kinga kali dhidi ya kirusi cha Omicron, kulingana na matokeo ya awali ya utafiti yaliyochapishwa Jumatano. Kampuni hiyo imesema vipimo vya maabara vimebainisha ongezeko la mara 25 la viwango vya kinga ya mwili. Hata hivyo, wametahadharisha kwamba chanjo mbili za awali huenda zisitoshe kuzuia maambukizi ya kirusi hicho.
Utafiti huo wa Pfizer bado unahitaji uchunguzi zaidi wa kisayansi, lakini unatoa taarifa ya kwanza juu ya ufanisi wa chanjo ya tatu dhidi ya Omicron. Ujerumani imeshuhudia ongezeko la uagizaji wa chanjo ya nyongeza ya BioNTech-Pfizer. Taasisi ya Ujerumani inayohusika na magonjwa ya kuambukiza ya Robert Koch (RKI) ilisema Jumatano kwamba asilimia 18.7 ya wakazi wa nchi hiyo wamepata chanjo ya nyongeza wakati serikali mpya ikiingia madarakani.