1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza yakanusha madai ya kuhujumu mabomba ya gesi

29 Oktoba 2022

Uingereza imekanusha vikali madai yaliyotolewa na Urusi kwamba wataalamu wake walihusika na mashambulizi ya mabomba mawili muhimu ya kusafirisha gesi barani Ulaya ya Nord Stream.

Dänemark Ostsee bei Bornholm | Leck Nord Stream 2
Picha: Danish Defence Command/AP/picture alliance

Wizara ya mambo ya kigeni ya Uingereza imesema madai hayo ya Urusi ikiwemo kuihusisha Uingereza na hujuma dhidi ya kamanda ya jeshi la majini la Urusi kwenye Bahari Nyeusi ni "uongo wa kiwango cha kutisha".

Kupitia ukurasa wa Twitter, wizara hiyo imesema "Ili kujiliwaza na kushindwa kwake katika uvamizi nchini Ukraine, wizara ya ulinzi ya Urusi imechagua njia ya kueneza uzushi wa kiwango kisicho na mfano".

Mapema leo Jumamosi, wizara ya ulinzi ya Urusi ilidaikikosi cha wataalamu wa jeshi la Uingereza kilichofanikisha mpango wa shambulizi la siku Jumamosi dhidi ya meli za Urusi kwenye rasi ya Crimea - ambayo Moscow iliinyakua kutoka Ukraine mnamo mwaka 2014- ndiyo kilitumika kufanya "shambulizi la kigaidi" kwenye mabomba ya Nord Stream 1 na 2 hapo Septemba 26.

Uingereza hata hivyo imesema "simulizi hizo za kubuni zinaonesha kile kinachojadiliwa kwa sehemu kubwa ndani ya serikali ya Urusi kuhusu mataifa ya magharibi".

Urusi yadai Uingereza imesaidia pia shambulizi dhidi ya meli zake za kivita

Mapema leo Jumamosi, jeshi la Urusi liliituhumu Ukraine kufanya shambulizi kubwa la ndege isiyo na rubani dhidi ya kamanda yake ya majini katika eneo la Bahari Nyeusi na kwenda mbali zaidi ikidai Uingereza iilisaidia Kyiv kufanikisha hujuma hiyo.

Picha: Vasily Batanov/AFP/Getty Images

Mji Mkuu wa rasi ya Crimea, Sevastopol ambao katika miezi ya karibuni umekuwa ukilengwa, ndiyo makao makuu ya kamanda hiyo meli za kivita za Urusi na eneo lake la kuandaa mipango katika vita nchini Ukraine.

Urusi ilidai imedungua ndege 16 zisizo na rubani katika shambulizi hilo dhidi ya bandari inayotumiwa na meli za kivita za Urusi huko Crimea.

Vikosi vya Urusi vimedai wataalamu wa Uingereza, ambao inasema wamepiga kambi kwenye mji wa kusini mwa Ukraine wa Ochakiv, walisaidia maandalizi na mafunzo kwa vikosi vya Ukraine kutekeleza shambulizi hilo.

Moscow imesema meli zilizolengwa kwenye shambulizi hilo la kambi ya Crimea zimekuwa zikitumika kutekeleza mkataba uliofikiwa chini ya Umoja wa Mataifa wa kufanikisha usafirishaji nje wa nafaka na bidhaa nyingine za Ukraine zilizokwama kutokana na mapigano.

Shambulizi la Crimea latajwa kuwa ndiyo kubwa zaidi kwenye rasi hiyo 

Picha: Russian Defense Ministry's press service/ZUMA/picture alliance

Gavana wa mji wa Sevastopol aliyewekwa madarakani na Urusi,   Mikhail Razvozhayev, amesema shambulizi la siku ya Jumamosi ni "kubwa kuliko yote" eneo hilo limewahi kushuhudia.

Madai ya Urusi kuhusu shambulizi hilo yametolewa wakati Jeshi la Ukraine limeripoti mapigano makali katika mikoa ya Luhansk na Donetsk mashariki mwa Ukraine, ikiwemo kwenye mji wa Bakhmut -- eneo ambalo vikosi vya Urusi vimesonga mbele katika wiki za karibuni.

Katika hatua nyingine, wapiganaji wanaotaka kujitenga na Ukraine na ambao wanaungwa mkono na Urusi wametangaza mabadilishano mapya ya wafungwa na serikali mjini Kyiv. Kila upande umetoa idadi ya wafungwa 50.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW