Uingereza yakataa kujiunga na mzingiro wa Hormuz
13 Aprili 2026
Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, alisema siku ya Jumatatu (Aprili 13) kwamba licha ya shinikizo kubwa kutoka utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani, kamwe nchi yake isingeliburuzwa kuingia kwenye vita dhidi ya Iran na wala kuunga mkono mzingiro wa Mlango Bahari wa Hormuz uliotangazwa na Trump.
"Ni muhimu sana kwa Mlango Bahari wa Hormuz kufunguliwa kikamilifu, na kwenye hilo tumewekeza juhudi zetu katika siku za hivi karibuni na tutaendelea kufanya hivyo, lakini sio kwa kutumia nguvu za kijeshi," alikiambia Kituo cha Radio 5 Live cha Shirika la Habari la Uingereza (BBC).
Kauli hiyo ya Uingereza, mshirika wa kijadi wa Marekani barani Ulaya, ilitolewa wakati kukiwa na taarifa kwamba tayari meli zilikuwa zimeacha kupita kwenye Mlango Bahari huo kufuatia kitisho cha Trump cha kuuzingira kabisa.
Meli hizo zilijizuwia kupita licha ya marekebisho na hakikisho la Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) kwamba mzingiro huo ungelihusisha meli zinazoingia na kutoka kwenye bandari na maeneo ya pwani ya Iran tu, na wala sio meli zinazokwenda au kutoka kwenye bandari nyengine za maeneo ya Ghuba.
IRGC: Tunaidhibiti Hormuz
Lakini Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi la Iran (IRGC) lilionya kwamba kusingekuwa na bandari hata moja kwenye "Ghuba ya Uajemi na Ghuba ya Oman itakayokuwa salama endapo bandari za Iran zitashambuliwa."
Jeshi hilo lilisema bado Mlango Bahari wa Hormuz ulikuwa kwenye udhibiti wake na kwamba meli zote zisizo kijeshi zilikuwa zinaruhusiwa kupita.
Hata hivyo, jeshi hilo lilisema meli yoyote ya kijeshi ingekabiliwa na hatua kali, baada ya kuchapisha video inayoonesha majibizano baina ya kikosi chake cha wanamaji (Sepah) na meli ya kijeshi ya Marekani, USS Frank E. Petersen Jr.
"Meli ya kivita 121. Hiki ni kituo cha jeshi la majini, Sepah. Lazima ugeuze safari na urudi kwenye Bahari ya Hindi haraka sana. Usipotii amri yangu, utashambuliwa." Inasikika sauti ya msemaji wa Sepah akionya kwenye video hiyo, huku yule wa meli ya Marekani akijibu: "Hii ni meli ya kivita ya muungano 121, ikiwa inapita kwenye njia ya bahari kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Haijakusudiwa kupambana nawe."
Baada ya majibizano mafupi, jeshi la Iran lilisema, meli hiyo ya Marekani iligeuza njia na kurudi ilikotoka.
Wasiwasi wa kuendelea vita
Mazungumzo ya kusitisha mapigano kati ya Marekani na Iran yalimalizika bila makubaliano mjini Islamabad, Pakistan, siku ya Jumamosi (Aprili 11), huku kila upande ukiulaumu mwengine kwa kushindwa huko.
Kuvunjika huko kwa mazungumzo ya Islamabad kumeongeza wasiwasi mpya wa kurudi kwenye vita vilivyokuwa vimedumu kwa siku 40 hadi siku vinasitishwa kupisha mazungumzo.
Kwenye ujumbe wake wa mwanzo tangu arejee Tehran, mkuu wa ujumbe wa Iran kwenye mazungumzo hayo, spika wa bunge, Mohammad Bagher Qalibaf, alimjibu Rais Trump wa Marekani kwamba endapo akianzisha tena vita, "tutapambana nawe."
Tayari bei za mafuta zimerudi kuwa za juu katika masoko ya dunia, ambapo asubuhi ya Jumatatu pipa moja lilikuwa linauzwa kwa dola 119 badala ya dola 70 ilivyokuwa kabla ya vita kuanza.