Uingereza yakataa kulipa malipo ya ziada ya bajeti
24 Oktoba 2014Maafisa wa Uingereza wamethibitisha leo(24.10.2014) ripoti iliyochapishwa katika gazeti la Financial Times kuwa taifa hilo limeombwa kuongeza mchango wake kwa asilimia 20 katika bajeti ya Umoja wa Ulaya.
Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron amelalamikia madai kutoka Umoja wa Ulaya kwamba nchi hiyo iongeze euro bilioni 2.1 ikiwa ni malipo ya nchi hiyo katika bajeti ya Umoja huo baada ya takwimu za kiuchumi kufanyiwa mapitio na kuonesha kuwa nchi hiyo ina uchumi mzuri zaidi.
Viongozi wa Umoja wa Ulaya , wanahangaika kupunguza athari zaidi za mzozo na Uingereza , wamekubaliana katika mkutano wao mjini Brussels kwamba mawaziri wao wa fedha watafanya mazungumzo ya dharura na halmashauri tendaji ya Umoja wa Ulaya kupitia upya tarakimu hizo katika wiki chache zijazo, wanadiplomasia wamesema.
Taarifa kutoka katika halmashauri kwenda kwa mataifa wanachama imeweka muda wa mwisho wa malipo hayo kuwa ni Desemba mosi mwaka huu.
Wapinzani wa Cameron ambao hawapendelei umoja wa Ulaya , wanaopata kuungwa mkono kwa haraka katika chama chake cha Conservative kabla ya uchaguzi wa Mei mwakani , wametumia kile maafisa wa Umoja wa Ulaya wanachosema , hatua isiyokuwa ya kawaida ya ongezeko hilo la mchango katika marekebisho ya mwaka.
Wanamshutumu waziri mkuu kwa kuwapotosha wapiga kura na Umoja wa Ulaya unafanya shughuli zake kama "mazimwi yenye kiu ya damu".
"David Cameron aliwahi kudai kwamba amepunguza bajeti ya Umoja wa Ulaya , lakini mchango wa Uingereza umeongezeka na kwa hivi sasa , mchango huo umeongezeka kwa mara ya pili. Ni kitu cha kuchukiza ," amesema Nigel farage , kiongozi wa chama cha Independence nchini Uingereza, ambacho kinataka Uingereza ijitoe kutoka katika Umoja wa Ulaya .
Hata washirika wa Cameron wa chama kinachopendelea muungano wa Ulaya cha Kiliberali, kinachoongozwa na waziri mkuu Nick Clegg, amesema "haikubaliki kupadilisha mchango wa mwanachama , wakati wowote tu."
Viongozi wengine kadhaa wa Umoja wa Ulaya hata hivyo wameitaka Uingereza kuheshimu sheria za muda mrefu za Umoja huo na kutoliweka zoezi hilo la vyombo vya mahesabu kuwa suala kubwa. Waziri mkuu wa Finland amesema Cameron hapaswi kulifanya suala hilo lionekane kama "mlima wakati ni kichuguu."
cameron amelieleza suala hilo katika siku ya pili ya mkutano wa Umoja huo na rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso amejibu kwamba sheria ni sheria na zinapaswa kuheshimiwa na sio kujaribu kujiuliza maswali.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape / rtre
Mhariri: Yusuf , Saumu