Uingereza yampokea Trump kwa 'mapambio'
17 Septemba 2025
Usiku wa kuamkia Jumatano (Septemba 17) ndipo Donald Trump na mkewe, Melania, waliposhuka ngazi za ndege ya Air Force One wakiwa wameshikana mikono na kulakiwa moja kwa moja na mkuu wa itifaki wa Uingereza, Monica Carllie, akiwa na Waziri wa Mambo wa Kigeni, Yvette Cooper, na Henry Hood, ambaye ni mwakilishi maalum wa Mfalme Charles III, sambamba na maafisa wengine wa usalama na wa serikali waliokuwa wamejipanga mstari katika Uwanja wa Ndege wa Stansted, London.
Baada ya mapokezi hayo mafupi, Trump na Melania walipanda helikopta maalum ya jeshi la anga la Marekani, ambayo iliwapeleka kwenye Nyumba ya Winflied, makaazi rasmi ya balozi wa Marekani nchini Uingereza, Warren Stephens.
Akiwa kwenye makaazi hayo, Trump alizungumza kwa kifupi na vyombo vya habari akielezea safari na matarajio yake makubwa kwa ziara hii ambayo amefika kwa mualiko rasmi wa Mfalme Charles, aliyemuita "rafiki wa muda mrefu na mtu anayependwa na kila mtu."
"Safari ilikuwa salama usalimini. Tunamshukuru balozi kwa kazi kubwa anayoifanya. Mahusiano baina ya nchi zetu ni mazuri sana. Namshukuru kwa kutukaribisha. Tulikuwa na safari nzuri na tumekuja na watu wengi. Kesho itakuwa sikukuu kwetu, nitakutana na Mfalme Charles." Alisema Trump.
Shangwe ya aina yake
Lakini ni mchana wa Jumatano, ndipo hasa ziara ya Trump ilipopangiwa kuanza kwa mapokezi makubwa kwenye Kasri la Windsor, makaazi rasmi ya Mfalme Charles na mkewe Camilla.
Hata hivyo, licha ya hatua kadhaa za kiusalama zilizochukuliwa kumuhakikishia faraja kiongozi huyo wa Marekani katika ziara yake hiyo, wanaharakati walifanikiwa kupachika bango kubwa lililoonesha picha ya Trump akiwa na Jeffrey Epstein, muhalifu wa mashambulizi ya ngono, ambaye alitiwa hatiani na kufia gerezani nchini Marekani.
Mkuu wa Polisi wa Thames Valley, Felicity Parker, alisema watu wanne wamekamatwa kwa tuhuma za kufanya mawasiliano yasiyo muafaka kutokana na ubandikaji wa bango hilo.
Katika Kasri la Windsor, jengo kongwe kabisa lenye miaka takribani 1,000 na ambalo bado linatumiliwa na wafalme, Trump alipangiwa kuingia kwa msafara wa magari ya farasi na kukaribishwa mchana huu kwa gwaride na bendi maalum na kisha kuhudhuria tafrija ya chakula.
Uingereza iliahidi kuwa hii itakuwa sherehe kubwa kabisa kuwahi kufanyika kumpokea kiongozi wa kigeni katika historia yake ya hivi karibuni.
Trump, mpenzi mkubwa wa ufalme, hajaweka siri hamu yake ya kuwa sio tu rais wa kwanza wa Marekani bali pia mwanasiasa wa kuchaguliwa kualikwa mara mbili na mfalme wa Uingereza kwa ziara rasmi.