1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiUingereza

Uingereza yatangaza sheria ya kuzuiwa maelfu ya wahamiaji

7 Machi 2023

Serikali ya Uingereza imetangaza sheria mpya inayokusudiwa kuzuwia maelfu ya wahamiaji wanaowasili nchini humo kwa boti ndogo ndogo kupitia ujia wa bahari unaofahamika kama English Channel.

UK Migranten kommen über den Ärmelkanal
Picha: Gareth Fuller/PA Wire/dpa/picture alliance

Serikali ya Uingereza imeeleza kuwa iko tayari kwa mapingamizi ya kisheria dhidi ya sheria hiyo, ambayo baadhi ya mashirika ya hisani ya wakimbizi yanasema inaweza kukosa mantiki na kufanya juhudi za maelfu ya wakimbizi wa kweli kuwa uhalifu.

Waziri Mkuu Rishi Sunakamefanya kuzuwia wahamiaji wanaowasili kwa boti kuwa mojawapo ya vipaumbele vyake vitano muhimu, baada ya idadi ya wahamiaji wanaowasili kwenye pwani ya kusini mwa Uingereza kuongezeka hadi zaidi ya 45,000 mwaka jana, ambapo karibu asilimia 90 waliomba hifadhi.

Soma pia:Kiongozi wa Scotland atangaza kujiuzulu

Sheria hiyo mpya itamaanisha kuwa mtu yeyote anayefika kwa njia hii atazuiwa kuomba hifadhi na kufukuzwa ama kurejeshwa katika nchi yake au kupelekwa kile kinachoitwa taifa la tatu ambalo ni salaama.

Waziri wa ndani kupewa jukumu la kuwafukuza wahamiaji haramu

Wahamiaji wakiwa katika fukwe ya bahari ya Gravelines Picha: SAMEER AL-DOUMY/AFP/Getty Images

Waziri wa Mambo ya Ndani Suella Braverman atapewa jukumu jipya la kisheria kuwafukuza wahamiaji haramu, na kutupilia mbali haki zao nyingine nchini Uingereza na sheria za haki za binadamu za Ulaya.

Akizungumza bungeni leo, waziri Bravermann amesema kwa serikali kutoshughulikia uhamiaji haramu itakuwa kusaliti matakwa ya watu waliochaguliwa kuwatumikia.

"Kinsingi haya ni maamuzi yanayoungwa mkono na Waingereza kwa usahihi kwa sababu yalikuwa maamuzi yaliyofanywa na Waingereza na wawakilishi wao waliochaguliwa, sio na wasafirishaji wa watu na wahalifu wengine wanaoingia Uingereza kila siku. Kwa serikali kutoshughulikia mawimbi ya wahamiaji haramu, wanaokiuka mamlaka ya mipaka yetu itakuwa kusaliti matakwa ya watu tuliochaguliwa kuwatumikia."

Serikali ya kihafidhina ya Sunak inashika mkia katika uchunguzi wa maoni ya wananchi na mada ya wahamiaji haramu inawagusa vibya wapiga kura na vyombo vya habari vya mrengo wa kulia, hasaa pale wanapovuka mataifa salaama ya Ulaya kabla ya kuingia Uingereza.

Lakini mashirika ya kutetea haki za binadamu na vyama vya upinzani vinasema mpango huo hautekelezeki na unawanyima fursa isivyo haki, wakimbizi walio hatarini. Christina Marriott, mkurugenzi mkuu wa mikakati wa Shirika la Msalaba Mwekundu la Uingereza, amesema Uingereza itakiuka majukumu yake chini ya mikataba ya kimataifa juu ya utoaji hifadhi.

Zaidi ya wahamiaji 3,000 wamewasili Uingereza mwaka huu 

Picha: PASCAL ROSSIGNOL/REUTERS

Zaidi ya wahamiaji 45,000 waliwasili kwenye fukwe za Kusini-Mashariki mwa Uingereza kwa boti ndogo mwaka jana, likiwa ongezeko la asilimia 60 kwa mwaka, kwenye njia ambayo imeongezeka umaarufu kila mwaka tangu 2018.

Takriban wahamiaji 3,000 wamewasili kufikia sasa mwaka huu, mara nyingi wakiishia kwenye hoteli za bei ghali zinazolipiwa na fedha za walipa kodi, na mrundikano wa maombi ya hifadhi sasa unazidi 160,000.

Soma pia:Uingereza: Tutafuata sera yetu kuwapeleka wahamiaji Rwanda 

Chini ya mpango huo mpya, wahamiaji haramu watahamishiwa kwenye kambi za kijeshi ambazo hazitumiki na serikali itaweka ukomo wa maombi ya kila mwaka ya hifadhi kwa kiwango kilichowekwa na bunge.

Hatari ya vivuko imetiliwa mkazo na mikasa kadhaa katika miaka ya hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na Novemba 2021 wakati watu wasiopungua 27 walipokufa baada ya mashua yao kupasuka.

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi