1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUingereza

Uingereza: Lawama zaongezeka kutokana na athari za Brexit

24 Novemba 2022

Waziri wa fedha wa Uingereza Jeremy Hunt ametetea hatua ya nchi yake ya kujiondoa Umoja wa Ulaya licha ya kuongezeka kwa lawama juu ya athari za kiuchumi zilizosababishwa na hatua hiyo ya Brexit.

Karikatur von Vladdo | Havladdorías

Waziri huyo wa fedha pia amekanusha madai kwamba analenga kuleta uhusiano wa karibu kati ya Uingereza na Umoja wa Ulaya. Waziri Hunt aliyepiga kura ya kutaka Uingereza ibakie kwenye jumuiya hiyo anatuhumiwa kuwa chanzo cha ripoti ya mwishoni mwa wiki iliyopita kwamba serikali ya Uingereza inakodolea macho uhusiano na Umoja wa Ulaya kama ule uliopo kati ya Uswisi na jumuiya hiyo.

Waziri wa fedha wa Uingereza Jeremy HuntPicha: PRU/AFP

Uswisi haimo katika Umoja wa Ulaya lakini ina mkataba wa biashara huru na jumuiya hiyo. Hata hivyo waziri huyo wa fedha wa Uingereza Jeremy Hunt amesisitiza kuwa yeye siye chanzo cha taarifa zilizonukuliwa kwenye vyombo vya habari kwamba Uingereza inataka uhusiano wa karibu na Umoja wa Ulaya.  

Soma Zaidi:Von der Leyen: Mianya mikubwa ingalipo kuhusu Brexit 

Waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Theresa May alipendekeza mpango kama huo, ambao ulikataliwa kabisa na wabunge, na ambao ulichangia kuanguka kwake mnamo mwaka 2019. Mrithi wa May, Boris Johnson, alivalia njuga mpango wake wa Uingereza kujiondoa kutoka kwenye Umoja wa Ulaya "Brexit” ulioungwa mkono na wabunge wengi kutokana na ushindi wake wa kishindo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2019 na hivyo kuifanya kampeni hiyo ikamilike. Lakini licha ya ahadi za uhuru zaidi za kuweka sera na kupanga mkondo wake ulimwenguni, Uingereza imeambulia maisha kuwa magumu mno baada ya Brexit, bila ya hata kuchanganya na msukosuko wa janga la Covid-19.

Waziri Mkuu aliyeondoka madarakani kinara wa Brexit Boris JohnsonPicha: Frank Augstein/AP Photo/picture alliance

Benki ya Uingereza na shirika huru la serikali la uangalizi wa matumizi zote zimesema mchakato wa Brexit umeuumiza uchumi wa Uingereza na kuuweka kwenye hatari ya kutumbukia kwenye mdororo. Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo limetabiri kuwa uchumi wa Uingereza utashuka chini zaidi kuliko nchi yoyote katika mataifa saba yaliyoendelea zaidi duniani kufikia mwaka ujao.

Wakosoaji wengi wamelaumu kwamba hali hiyo ni kutokana na hatua ya Brexit, ambayo ilisababisha Uingereza kujiondoa kutoka kwenye soko la pamoja la Ulaya na kwenye umoja wa forodha, hatua ambazo zilisitisha harakati zote za maingiliano huru kati ya nchi wanachama.

Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi SunakPicha: Peter Nicholls/REUTERS

Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak alisisitiza kwamba utawala wake hauna nia ya kufufua uhusiano wowote na Umoja wa Ulaya ambao unaegemea sheria za Umoja huo huku wabunge wanaounga mkono Brexit wakionya kuhusu hatua zozote za kurudi nyuma.

Tume ya Umoja wa Ulaya kwa upande wake imesema hakuna mpango uliopo mezani kuhusu kufikiwa makubaliano na Uingereza kama yaliyopo kati ya Umoja wa Ulaya na Uswizi.

Chanzo: AFP

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW