1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingerezea imepokea Urais wa Umoja wa Ulaya

Lillian Urio30 Juni 2005

Kiuanzia leo, Uingereza itapokea uongozi wa Urais wa Umoja wa Ulaya, kwa kipindi cha miezi sita. Kwa kipindi hicho Waziri Mkuu Tony Blair atawakilisha nchi yake katika nafasi hiyo ya Umoja huo. Watu wa Ulaya watafuatilia kwa makini kipindi hiki cha uongozi, kutokana na kwamba uhusiano wa Uingereza na Umoja wa Ulaya, hapo awali ulikuwa na misukosuko.

Waziri Mkuu wa Uingereza Tony Blair akizungumza na Bunge la Umoja wa Ulaya
Waziri Mkuu wa Uingereza Tony Blair akizungumza na Bunge la Umoja wa UlayaPicha: AP

Waziri Mkuu wa Luxenburg, Jean-Claude Juncker na mwenzake wa Ufaransa, Jacque Chirac, walimshutumu Waziri Tony Blair kuwa chanzo cha matatizo ya mkutano mkuu wa Umoja wa Ulaya. Mkutano huo ulikuwa na lengo la kutatua matatizo yaliojitokeza katika Umoja huo.

Walisema Waziri Blair ni Mwingereza ambaye ni adui wa Umoja wa Ulaya. Lakini katika bunge la Umoja huo Waziri Blair alifanya kazi nzuri ya kujionyesha kuwa mshabiki mzuri wa Umoja huo. Akisema Ulaya ina umuhimu kwake, zaidi ya kuwa sehemu ya kufanyia biashara tu na hataki kuharibu utaratibu wa kijamii wa Umoja huo.

Viongozi wenzake wamesema watapima ubora wa utawala wake, kama rais wa Umoja huo, kwa matendo yake na kuangalia kama yatafanan na maeneo yake.

Waziri huyo wa Uingereza anapo pokea uskani wa Umoja wa Ulaya, wanadiplomasia wengi mjini Brussels, kwenye makao makuu ya Umoja huo watakuwa wanaogopa wimbo kutoka Uingereza wa Rule Britania, ukimaanisha, Uingereza Tawala.

Waziri Blair, alivyoongea na wandishi wa habari mara ya mwisho mjini Brussels alijaribu kueleza kwamba lengo lake sio Uingereza Kuutawala Umoja huo. Malengo yake ni tofauti kabisa, anataka kutafuta suluhisho ya matatizo, mfano ule wa katiba au ule wa masuala ya kifedha ya Umoja huo, kwa kuanza na majadiliano.

Waziri Blair amesema:

“Nadhani ni majadiliano mazuri. Ni wazi kwamba majadiliano kama haya yanaendelea katika kila nchi ya Ulaya, pamoja na Ufaransa. Kwa hiyo ahca tujadiliane. Mimi sidhani kama nitapata kipaumbele kwenye majadiliano hayo, nataka tuyaanze”.

Waziri Juncker, aliyekuwa Rais wa Umoja wa Ulaya kwa kipindi kilichopita, alimlaumu Waziri Blair kwamba alisababisha matatizo ndani ya Umoja huo kwa makusudi, Waziri Blair hazingati lawama hizo.

Anachokizingatia ni fedha za Umoja huo zitumike ipasavyo. Sio kwa ajili ya kilimo na kusaidia ujenzi tu, bali pia, kwa ajili ya utafiti, maendeleo na uvumbuzi. Katika kipindi chake cha Urais, Waziri Blair hataki kuufuta Umoja wa Ulaya wala kufanya mageuzi makubwa ya mfumo wa kijamii wa Ulaya, kama vile Kansela Schroder wa Ujerumani alvyodai atafanya.

Waziri Blari ameeleza:

“Jinsi ya kuwalinda watu ni kutumia mbinu kama uwekezaji katika vitu nilivyovitaja, katika ujuzi, uwekezaji katika elimu na kuunda sekta ya vyuo vikuu vyenye ubora sawa na vyovyote duniani. Ina husu sera ya kijamii, inavyowasaidia watu kupata ujuzi na kazi. Vitu vyote hivi havimaanishi kwamba tunaacha kulinda jamii, bali tunabadilisha mfumo ili uendane na hali halisi ya wakati huu. Kama hatutafanya hivyo, matokeo yake ni hali yetu ya maisha itashuka ”.

Waziri Blair anaamini kwamba, wananchi wa Ufaransa na Uholanzi, waliopinga katiba ya Umoja huo, wanawasiwasi juu ya utandawazi na wanahitaji majibu mapya juu ya sualal hilo.

Alisema ni muhimu kuanza kushughulikia wasiwasi wa watu. Ili wananhci waone viongozi wao wanaeleka wapi. Waziri Blair anasumbuliwa na tendo la uundaji wa tume, kila mara, wa kutatua matatizo. Kinachomshangaza ni kwamba, suluhisho likipatikana halizingatiwi.

Kuna wanasiasa wengi wanao furahia kwamba Waziri Blair anampango wa kutafuta suluhisho la tatizo la suala la fedha la Umoja huo. Hata kamishna wa viwanda wa Ujerumani Gunter Verheugen angependa kuona Waziri Blair analeta mabadiliko.

Kwa maoni yake, wakati umefika wa kutumia fedha kwa vitu wanavyovihitaji. Kwa mfano kwa kukuza uchumi, ajira na masuala ya uvumbuzi.

Suala la Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya utaangukia kipindi chake cha uongozi, naye Waziri Blair anaunga mkono jambo hili. Wakti huo huo, wananchi wengi wa Uingereza hawajali kwamba Waziri Mkuu wao anakuwa Rais wa Umoja wa Ulaya. Wanasema hawafikirii sana juu ya suala hilo na wanaona kama halitawaletea mabadiliko makubwa katika maisha yao.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW