Ujasusi wa Marekani wapandisha hasira
10 Julai 2014Katika siku ya pili ya majadiliano mjini Washington, ujumbe wa bunge la Ujerumani umesema kwamba kashfa hii mpya ya ujasusi inaweza kusababisha mgawanyiko wa kudumu kati ya washirika hao wawili.
Akizungumza na waandishi wa habari katika jengo la ubalozi wa Ujerumani mjini Washington, mwenyekiti wa kamati ya mambo ya nje ya Bunge la Ujerumani, Norbert Roettgen, ameonya juu ya kile alichokiita "mgogoro wa chini kwa chini" kati ya nchi yake na Marekani.
Roettgen amewaambia waandishi hao kadhia hizi mbili zimesababisha madhara makubwa sana kwa mahusiano kati ya nchi yake na Marekani, na kwamba haoni dalili yoyote ikiwa Marekani itabadili msimamo wake hivi karibuni.
Ujerumani inataka Marekani isaini makubaliano ya kutokufanyiana ujasusi, lakini Roettgen amesema hilo "si jambo lenye uhalisia" kwa Marekani.
Marekani yataka mazungumzo
Hata hivyo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani, Martin Schaefer, amesema kwamba tayari Marekani imeonesha nia ya kulizungumzia suala hili kwa upana zaidi. "Balozi wa Marekani ameelezea nia ya kuzungumzia maswali haya na mwakilishi wa Wizara yetu ya Mambo ya Nje, nasi pia tulitaka kuzungumza naye," alisema Schaefer.
Ujumbe huo wa Bunge la Ujerumani, Bundestag, uko nchini Marekani kujadiliana hatima ya mahusiano kati ya pande hizo mbili, chini ya kivuli cha ukosefu wa kuaminiana uliozushwa na kashfa hizo za ujasusi.
Mjini Berlin, wizara ya ulinzi ya Ujerumani imeanzisha uchunguzi wa pili wa ujasusi, baada ya wiki iliyopita kukamatwa kwa mfanyakazi wa Shirika la Usalama wa Ndani (BND) akishukiwa kuitumikia pia CIA. Msemaji wa wizara hiyo, Kanali Uwe Roth, amethibitisha kufanyika kwa uchunguzi huo.
"Ninaweza kuthibitisha kwamba kuna uchunguzo wa Ofisi ya Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali ya Shirikisho ambao uko chini ya wizara ya ulinzi. Siwezi kusema mengi zaidi lakini naweza kuwaambia kwamba tunaichukulia kesi hii kwa umakini mkubwa," Rothaliwaambia waandishi wa habari.
CIA haikumfahamisha Obama
Gazeti la New York Times linasema hata Rais Barack Obama hakujulishwa na CIA juu ya kadhia hii, ingawa alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani siku ya tarehe 3 Julai.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, hivi sasa maafisa wa Ikulu ya Marekani wanahaha kumsaka afisa wa CIA aliyekuwa dhamana wa kadhia hiyo kujua ni kwa nini hakuijulisha Ikulu hiyo.
Ujumbe wa bunge la Ujerumani ulio Marekani tayari umeshakutana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Victoria Nuland, na mwenyekiti wa Kamati ya Ujasusi ya Senate, Dianne Feinstein.
Binafsi Feinstein anatafautiana sana na CIA, ambayo mapema mwaka huu aliituhumu kwa kuingilia uchunguzi wa bunge juu ya programu ya uwekaji kizuizini na kuwahoji washukiwa chini ya utawala wa George Bush.
Mhariri: Yusuf Saumu