Ujenzi wa kambi ya kijeshi Urusi
5 Agosti 2014Gazeti la "Saarbrücker Zeitung" linasema: Gabriel anataka kuonyesha amechukua hatua ya kisiasa lakini uamuzi wake una kasoro: Zaidi ya watu laki moja wameajiriwa katika sekta ya utengenezaji wa silaha hapa Ujerumani. Gabriel hawezi kujifanya kuwa hajali kuhusu ajira hizo kwani kampuni iliyotaka kujenga huko Urusi sasa inaweza kudai fidia kutoka kwa serikali.
Mhariri wa gazeti la "Thüringishe Landeszeitung" kwa upande wake anasema kuwa suala la ajira haliwezi kuwa sababu ya kukubali kila aina ya biashara na nchi yoyote ile. Mhariri wa gazeti hilo anasisitiza kuwa nchi kama Ujerumani inayoongoza kwa uuzaji wa silaha lazima iwe tayari kupoteza ajira kama hatua hiyo itasaidia kuleta amani duniani.
Maadhimisho ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia.
Gazeti la "Kieler Nachrichten" linaandika: Mapigano yanayoendelea sehemu mbali mbali za dunia yanaonyesha kuwa ulimwengu bado haujapata fundisho la kutosha. Vita kuu zimeonyesha kwamba taifa linalokiuka haki za binadamu au kutumia nguvu litalazimika kupambana na jumuiya ya kimataifa.
Mhariri wa gazeti la "Leipziger Volkszeitung" anauliza kama vita vingine vinatishia kutokea Ulaya hivi karibuni. Mhariri huyo anaendelea kwa kusema: Vita kuu ya kwanza na athari zake bado ziko kwenye kumbukumbu za viongozi wa nchi za Ulaya. Hivyo viongozi hao watafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba mapigano katika eneo moja hayasambai na kuwa vita katika bara zima.
Mwandishi: Elizabeth Shoo/Inlandspresse
Mhariri: Josephat Charo