Ujerumani: Bado hakuna mwafaka wa kupeleka vifaru Ukraine
20 Januari 2023Marekani na Ukraine wote wamesema ni vyema idhini hiyo ikatolewa kwa haraka ila Ujerumani inashikilia kwamba itapeleka vifaru hivyo iwapo tu patakuwa na maafikiano kutoka kwa nchi zote marafiki.
Mazungumzo ya mawaziri wa ulinzi katika kambi ya kijeshi ya Marekani ya Ramstein nchini Ujerumani Ijumaa, yanafuatia onyo kutoka kwa Ukraine kwamba Urusi inataka kuzidisha mashambulizi yake baada ya kuzingira sehemu za Ukraine mashariki na kusini ambazo haina udhibiti kamili.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy, amewashukuru marafiki wa Ukraine ila akasema msaada zaidi unahitajika tena kwa haraka, kauli iliyoungwa mkono na waziri wa ulinzi wa Marekani, Lloyd Austin.
"Huu si wakati wa kupunguza kasi, ni wakati wa kuchimba chini zaidi. Waukraine wanatutazama, Ikulu ya Kremlin inatutazama na historia inatutazama," alisema Austin.
Hakuna mwafaka wa kupeleka vifaru Ukraine
Kwa upande wake waziri wa ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius ambaye nchi yake inakabiliwa na shinikizo la kutoa idhini ya vifaru chapa Leopard 2 kupelekwa Ukraine, amekanusha kwamba Ujerumani inazuia kupelekwa kwa vifaru hivyo akisema serikali ya Ujerumani, itakuwa tayari kulitekeleza hilo kwa haraka iwapo kutakuwa na makubaliano miongoni mwa nchi marafiki.
Pistorius ameongeza kwamba kwa sasa hakuna uamuzi uliofikiwa kuhusiana na kuvipeleka vifaru hivyo vyenye nguvu nchini Ukraine.
"Na tumezungumzia pia uwezekano wa kutumwa kwa vifaru aina ya Leopard. Kwanza kabisa, lazima niseme wazi wazi, hatuna maoni sawa katika hilo," alisema Pistorius.
Pistorius lakini amesema kipau mbele cha Ujerumanikwa Ukraine ni mifumo ya angani ya kujilinda na kwamba Ujerumani haitosita kuisaidia Ukraine.
Ulaya itajutia uamuzi wa kuipa vifaru Ukraine
Waziri huyo wa ulinzi wa Ujerumani lakini amesema ameiagiza wizara yake kuangalia akiba ya vifaru hivyo ili hatua mwafaka zichukuliwe kwa haraka iwapo uamuzi utafikiwa wa kuviwasilisha Ukraine.
Urusi imesema kuisaidia Ukraine na vifaru ni jambo ambalo halitosaidia na kwamba nchi za Magharibi zitajutia "ndoto" yake kwamba Ukraine inaweza kushinda katika uwanja wa mapambano.
Naye Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Jens Stoltenberg aliyehudhuria mkutano huo wa Ramstein pia, amesema, nchi zinazoiunga mkono Ukraine hazistahili tu kuzingatia kutuma silaha mpya huko Kyiv ila kutazama zana za mifumo ya zamani na kusaidia kuikarabati.
Chanzo: Reuters/AFP/AP