1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani: Chanjo ya COVID-19 kuanza Januari

7 Desemba 2020

Ujerumani imesema chanjo ya virusi vya corona itaanza kutumika nchini humo mwanzoni mwa Januari, 2021.

Biontech Covid-19 Impfstoff
Picha: NurPhoto/picture alliance

Mkuu wa wafanyakazi wa serikali ya shirikisho ya Ujerumani, Helge Braun amesema chanjo ya virusi vya corona itaanza kutumika siku za mwanzo za Januari. Braun ambaye ni daktari, ameliambia gazeti la Bild kwamba yeye mwenyewe amejiandaa kusaidia katika kutoa chanjo hiyo.

Amesema yeye pamoja na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel watachomwa chanjo ya virusi vya corona wakati muda wao utakapofika. Leo, taasisi ya kudhibiti magonjwa ya kuambukiza ya Ujerumani, Robert Koch, imerekodi maambukizi mapya 12,332 ya virusi vya corona ndani ya muda wa saa 24, ikilinganishwa na visa 11,168 wiki iliyopita. Aidha, taasisi hiyo imerekodi vifo vipya 147.

Soma zaidi: Merkel awataka Wajerumani kuendelea kutii vizuizi vya kudhibiti corona

Mjini Dusseldorf polisi imesema mamia ya watu waliandamana kupinga hatua zilizowekwa kuzuia kusambaa kwa COVID-19, ingawa pia walikumbana na mamia ya waandamanaji wengine wanaounga mkono hatua hizo.

Bavaria kuongeza masharti

Wakati huo huo, kuanzia siku ya Jumatano jimbo la Bavaria linapanga kuweka amri ya kutotoka nje kwenye maeneo yaliyoathirika zaidi na COVID-19, hata wakati wa sikukuu ya Mwaka Mpya. Jimbo la Thuringia pia linafikiria kuchukua hatua kama hiyo. Waziri Mkuu wa Jimbo la Bavaria, Markus Soeder amesema leo kuwa Kansela Merkel na wakuu wa majimbo ya Ujerumani wanapaswa kukutana kabla ya sikukuu ya Krismasi kujadiliana kuhusu hatua kali zaidi za kuchukua kuzuia kuenea kwa virusi hivyo, kwani mfumo uliopo sasa hautoshi.

Kansela Angela Merkel akihudhuria moja ya mikutano ya serikaliPicha: Markus Schreiber/AP/picture alliance

''Kila dakika nne mtu mmoja anakufa kwa corona Ujerumani. Kila dakika nne. Bavaria ni kila baada ya dakika 20. Ndani ya wiki moja tu, watu 474 wamekufa kwa corona Bavaria. Tuhanitaji kuchukua hatua madhubuti sasa,'' alifafanua Soeder.

Huku hayo yakijiri, Umoja wa Ulaya unatarajiwa kufanya maamuzi ifikapo Desemba 29 kuhusu kuidhinisha chanjo ya kwanza ya COVID-19 kwa ajili ya matumizi. Tayari Ujerumani imeanza kuandaa vituo maalum kwa ajili ya chanjo.

Korea Kusini yaamuru upimaji zaidi

Kwengineko waziri wa afya wa Korea Kusini amelielezea eneo moja kwenye mji mkuu, Seoul kama eneo lenye maambukizi makubwa ya COVID-19, wakati ambapo Rais Moon Jae-in ameamuru kuongezwa kwa huduma za kuwapima watu.

Rais mteule wa Marekani, Joe Biden anatarajiwa kumteua Mwanasheria Mkuu wa California, Xavier Becerra kuwa waziri wa afya na huduma za kibinaadamu. Hatua hii inaonesha kuwa Becerra, mwenye umri wa miaka 62 atachukua nafasi muhimu katika mapambano dhidi ya janga la COVID-19.

Aidha, Qatar imesema ina uhakika kwamba mashindano ya Kombe la Dunia yataendelea kama ilivyopangwa mwaka 2022, baada ya kufanikiwa kwa utoaji wa chanjo ya COVID-19. Na huko nchini Australia ndege ya kwanza ya kimataifa imetua leo kwenye mji wa Melboure tangu mwezi Juni.

(AP, AFP, Reuters)

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi