Ujerumani, Finland zashinikiza misaada kuingia Gaza
28 Mei 2025
Kansela Friedrich Merz wa Ujerumani, ambaye katika siku za hivi karibuni amekuwa akiikosowa vikali Israel, amesema misaada ya kibinaadamu lazima iruhusiwe kuingia Gaza "haraka sana".
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Turku akiwa na mwenyeji wake, Waziri Mkuu wa Finland, Petteri Orpo, Merz alisema lazima "tuishinikize Israel kuhakikisha kuwa msaada unawafikia kweli walengwa. Lakini pia ni muhimu pia kwamba Hamas haizuwii misaada kuwasili."
"Tulichokiona Gaza hakikubaliki kwa namna yoyote ile. Lazima mauaji na mateso kwa raia yakomeshwe." Aliongeza kansela huyo wa Ujerumani.
Soma zaidi: Ujerumani yatishia hatua dhidi ya Israel katika mabadiliko ya msimamo kuhusu Gaza
Kwa upande wake, Waziri Mkuu Orpo alitilia mkazo ulazima wa misaada ya kibinaadamu kuingia Gaza, akisema hali iliyopo kwenye Ukanda huo ni janga baya kabisa la kibinaadamu na lazima likabiliwe ipasavyo.
Sweden yamuita balozi wa Israel
Taifa jirani la Sweden hapo jana lilimuita balozi wa Israel kwenye wizara ya mambo ya nchi hiyo ya Nordic, na kumtolea wito kwa Israel kuhakikisha inaondosha haraka vikwazo vinavyozuwia misaada ya kibinaadamu kuingia Gaza.
Kwenye taarifa yake, wizara hiyo ya mambo ya kigeni ya Sweden ilitaja haki ya Israel kujilinda lakini ikasema jinsi vita vinavyoendeshwa kwenye Ukanda wa Gaza haikubaliki.
"Israel inapaswa kutimiza wajibu wake wa kuwalinda raia na miundombinu ya kiraia kwa mujibu wa sheria za kimataifa." Ilisema taarifa hiyo.
Soma zaidi: Kansela Merz aikosoa Israel kwa inachofanya Gaza
Hayo yakijiri, serikali ya Ireland iliridhia hapo jana rasimu ya sheria ya kupiga marufuku uingizaji wa bidhaa kutoka makaazi ya walowezi wa Israel yanayozingatiwa na sheria za kimataifa kuwa haramu, hatua ambayo haikuwahi kutazamiwa kwamba ingechukuliwa na mwanachama wa Umoja wa Ulaya.
Hatua hii inafuatia uamuzi wa mwaka jana wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki kwamba ukaliaji wa Israel dhidi ya Ukingo wa Magharibi, Jerusalem Mashariki na Ukanda wa Gaza ni haramu chini ya sheria za kimataifa.
Umoja wa Ulaya watakiwa kuifuata Ireland
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ireland aliliambia shirika la habari la AFP kwamba serikali ya nchi hiyo imekubali kuwasilisha sheria inayopiga marufuku biashara yoyote na maeneo yanayokaliwa kimabavu ndani ya mamlaka ya Palestina, ikiamini kwamba huo ni wajibu wake wake mbele ya sheria ya kimataifa.
Maeneo hayo yanajumuisha makaazi ya watu, mashamba na makampuni yaliyo nje ya eneo linalotambuliwa kimataifa kuwa ni mamlaka ya Israel. Kabla ya uamuzi wa baraza la mawaziri, Waziri wa Mambo ya Nje na Naibu Waziri Mkuu wa Ireland, Simon Harris, aliwaambia waandishi wa habari mjini Dublin kwamba anatazamia mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya yatafuata mfano wa nchi yake.
Soma zaidi: Ujerumani yaikosoa Israel kwa vita vyake huko Gaza
Mwezi Mei mwaka jana, Ireland pamoja na Uhispania, Norway na mwezi mmoja baadaye, Slovenia, ziliitambua Palestina kuwa ni taifa kamili, uamuzi uliopelekea mzozo wa kidiplomasia na Israel.
Mwezi uliopita, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alitangaza kuwa Paris nayo itachukuwa hatua kama hiyo mapema mwezi ujao wa Juni.
Uamuzi wa jana wa Ireland unakuja ikiwa ni wiki moja tu baada ya Umoja wa Ulaya kuamuru mapitio mapya ya Makubaliano ya Ushirikiano na Israel, mkataba uliosainiwa mwaka 1995 ambao unajenga msingi wa mafungamano ya kibiashara baina ya pande hizo mbili.
Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, alisema sehemu kubwa ya mataifa wanachama 27 kwenye mkutano wa mawaziri wa mambo ya kigeni wa Umoja huo waliunga mkono hatua hiyo ikiwa na lengo la kuiwekea mbinyo Israel.