1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UhalifuUjerumani

Ujerumani: Gari laparamia watu soko la Krismasi Magdeburg

20 Desemba 2024

Watu wasiopungua wawili wameripotiwa kufariki, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Ujerumani. Msemaji wa serikali ya mkoa amelielezea tukio hilo kama shambulio, na kumtaja mshukiwa kuwa raia wa Saudi Arabia.

Gari laparamia watu kwenye soko la Krismas Magdeburg, nchini Ujerumani.
Polisi imemtia mbaroni raia wa Saudi Arabia mwenye umri wa miaka 50 akishukiwa kuhusika na shambulio hilo.Picha: Dörthe Hein/picture alliance/dpa/dpa-Zentralbild

Gari liliuparamia umati wa watu katika soko la Krismasikatika mji wa Magdeburg, katikati mwa Ujerumani, Ijumaa usiku.

Watu wasiopungua wawili wameuawa, akiwemo mtoto mdogo, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Ujerumani.

Msemaji wa jiji, Michael Reif, alisema kuwa "watu wengi wamejeruhiwa."

Polisi wamemkamata dereva wa gari hilo, kulingana na vyanzo vya serikali ya mji vilivyonukuliwa na shirika la habari la dpa la Ujerumani.

Soma pia: Ujerumani yamtafuta mshukiwa raia wa Tunisia

Mamlaka zimelifunga soko la Krismasi na huduma za dharura ziko eneo la tukio.

Msemaji wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Magdeburg ameiambia dpa kuwa waathiriwa wa kwanza 10-20 tayari wamewasili hospitalini, akiongeza kuwa, "Tunaendelea kujiandaa [kwa zaidi]. Vitanda vya wagonjwa mahututi viko tayari."

Mwanaume aliyekamatwa kufuatia shambulio hilo hakuwa akijulikana kwa vyombo vya usalama kama mfuasi wa itikadi kali, kwa mujibu wa vyanzo vya usalama vilivyozungumza na shirika la habari la dpa.

Wafanyakazi wa huduma za dharura wakiwa zamu kwenye hema kuwahudumia majeruhi katika soko la Krismasi huko Magdeburg.Picha: Heiko Rebsch/dpa/picture alliance

Kwa mujibu wa uchunguzi wa awali, mwanaume huyo anasemekana kuwa na umri wa miaka takriban 50 na anatoka Saudi Arabia.

Tukio la Ijumaa limeibua kumbukumbu za shambulio la mwaka 2016 katika soko la Krismasi mjini Berlin. Shambulio hilo, lililotekelezwa na mshambuliaji mwenye itikadi kali kwa kutumia lori lililoibwa, liliua watu 13 na kuwajeruhi zaidi ya 70.

Wanasiasa wa serikali ya mkoa na shirikisho wanena

"Hili ni tukio la kusikitisha sana, hasa katika siku hizi kabla ya Krismasi," alisema Waziri Mkuu wa jimbo la Saxony-Anhalt, Reiner Haseloff, alipokuwa akielekea Magdeburg.

Msemaji wa serikali ya mkoa, Matthias Schuppe, alisema anatilia shaka kuwa tukio hilo lilikuwa shambulio.

Soma pia: Msako wa mtuhumiwa wa Berlin waghadhibisha raia

Friedrich Merz, mgombea wa Ukansela wa chama cha kihafidhina cha CDU, alisema amesikitishwa na habari kutoka Magdeburg.

"Fikra zangu ziko kwa waathiriwa na familia zao. Ningependa kuwashukuru wote wanaotoa huduma za dharura kwa kuwahudumia majeruhi katika eneo la tukio," alisema.

Huduma za dharura, polisi na idara za zima moto ziko kazini katika soko la Krismasi mjini Magdeburg.Picha: Heiko Rebsch/picture alliance/dpa

Naibu Kansela Robert Habeck pia alielezea mshtuko wake kutokana na "habari mbaya kutoka Magdeburg, ambapo watu walitaka kusherehekea msimu wa Advent kwa amani na mshikamano. Fikra zangu ziko kwa waathiriwa na familia zao."

Kansela Olaf Scholz alitoa maoni yake kupitia X, akisema "habari kutoka Magdeburg zinaashiria hali mbaya zaidi." Pia alitoa shukrani zake kwa wahudumu wa dharura wa kwanza.

Magdeburg, mji uliopo magharibi mwa Berlin, ni mji mkuu wa jimbo la Saxony-Anhalt na una takriban wakazi 240,000.

Chanzo: Mashirika

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW