1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Scholz: Hatutakubali amani ya Ukraine iamuliwe na Urusi

Angela Mdungu
20 Machi 2024

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema Urusi inaonesha dalili za udhaifu na haina nguvu kama inavyofikiriwa.

Ujerumani | Hotuba ya Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz
Kansela wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: Liesa Johannssen/REUTERS

Katika tamko lake kiongozi  huyo wa Ujerumani pia amezungumzia juu ya Mashariki ya Kati na anatumai kwamba Umoja wa Ulaya utafikia mwafaka.

Juu ya vita vya Ukraine Kansela Olaf Scholz amesisitiza dhamira  ya nchi yake pamoja  na ya Umoja wa Ulaya ya kuendelea kuisaidia Ukraine kwa kadri itakavyohijatika. Amewaambia wabunge kuwa Rais wa Urusi Vladmir Putin amefanya makosa ikiwa anadhani kwamba Ujerumani itaacha kuiunga mkono Ukraine.

Soma zaidi:Bunge la Ujerumani lakataa kuitumia Ukraine makombora ya masafa marefu 

Scholz, ambaye pia amepinga upelekaji wa makombora ya masafa marefu aina ya Taurus nchini Ukraine, hata hivyo amesema kuwa Ujerumani imedhamiria kuisaidia Ukraine kujilinda dhidi ya hila za Putin.

Mipaka haipaswi kusogezwa kwa mabavu

Kansela Scholz ameongeza kuwa hawatokubali amani ya Ukraine iamuliwe na Urusi na kusisitita kuwa mipaka haipaswi kusogezwa kwa mabavu.

Katika hotuba yake Kansela huyo wa Ujerumani amesesema kuwa sheria ina nguvu kuliko machafuko na kwamba Putin alitaka kulibadilisha hilo kwa kuishambulia Ukraine.

Rais wa Urusi, Vladmir PutinPicha: Maxim Shemetov/REUTERS

Zaidi ameelezea udhaifu wa Urusi kwa kuainisha kile alichokiita dhulma za uchaguzi katika taifa hilo na shinikizo dhidi ya upinzani, mambo ambayo ameyataja kuwa ni dalili ya udhaifu.

Hayo yanajiri wakati kukiwa na uhitaji wa kuchukua hatua za haraka kuisaidia Ukraine ndani ya Umoja wa Ulaya wakati nchi 27 wanachama wa zikijiandaa na mkutano wa kilele wa Ijumaa huku Ukraine ikiripotiwa kuwa na akiba ndogo ya silaha.

Soma zaidi: Scholz asisitiza msimamo wake wa kutoipa Ukraine makombora ya Taurus

Duru za habari zinasema, Umoja wa Ulaya umezuia fedha za Urusi karibu dola za kimarekani bilioni 210 nyingi kati ya hizo zikiwa kwenye benki za Ubelgiji, hatua inayotafsiriwa kuwa ni kulipa kisasi cha vita vya Moscow dhidi ya Ukraine.

Katika hatua nyingine, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ametoa wito wa kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza sambamba na kuachiliwa kwa mateka wanaoshililiwa na wapiganaji wa kundi la Hamas na makundi mengine ya wanamgambo wa Kiislamu. Scholz amesema kuwa msaada zaidi wa kiutu unapaswa kufika katika ukanda huo. Kundi la Hamas limeorodheshwa na Marekani, Israel pamoja na Umoja wa Ulaya kuwa ni la kigaidi.