1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani haitaongeza kikosi cha jeshi Afghanistan, Merkel

11 Mei 2017

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema Ujerumani itaendelea kuongoza mafunzo ya wanajeshi wa muungano wa kujihami wa NATO kaskazini mwa Afghanistan, lakini haina lengo la kuongeza wanajeshi wake katika eneo hilo.

Deutschland Merkel empfängt Stoltenberg
Katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg na Kansela Angela MerkelPicha: Getty-Images/AFP/T. Schwarz

Kansela Merkel vile vile amesema pia Ujerumani haina nia ya kuongeza jukumu lake pia katika vita dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS.

Merkel atakuwa anawania muhula wa nne kama Kansela katika uchaguzi wa kitaifa mwezi Septemba, huku Wajerumani wengi wakiwa na wasiwasi kuhusiana na idadi ya wanajeshi wanaotumwa katika mataifa ya kigeni, ikizingatiwa kuwa Ujerumani ni taifa ambalo liliwahi kuongozwa katika misingi ya kijeshi na kuweka maslahi yake mbele.

Akizungumza katika kikao cha pamoja cha waandishi wa habari na Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg, Merkel alisema atasubiri kuona matokeo ya uchunguzi wa NATO kuhusiana na ombi la kitengo cha jeshi cha uongozi wa muungano huo, la kutuma vikosi zaidi Afghanistan.

Nchi wanachama wa NATO watakutana Mei 25

Lakini kiongozi huyo aliashiria kwamba Ujerumani haiko tayari kuchukua majukumu zaidi katika suala hilo.

"Nasubiri maamuzi lakini sidhani kwamba sisi ndio wa kwanza kuongeza idadi yetu huko," alisema Merkel, "tunastahili kujali zaidi kuhusiana na kustawisha usalama kaskazini mwa nchi hiyo."

Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Getty Images/AFP/A. Nemenov

Naye Katibu Mkuu wa NATO Stoltenberg, alisema anatumai nchi wanachama wa muungano huo watakapokutana Mei 25, kutafikiwa uamuzi wa iwapo muungano huo ujiunge kikamilifu na muungano unaoongozwa na Marekani unaopambana na kundi linalojiita Dola la Kiislamu.

Marekani chini ya rais Donald Trump, inataka msisitizo zaidi uwekwe kwa NATO kupambana na ugaidi. Stoltenberg alisema tayari wanachama wote 28 wa NATO ni wanachama wa muungano dhidi ya IS, ingawa NATO yenyewe si mwanachama rasmi. Alisema swali ni iwapo NATO yenyewe inastahili kuwa katika meza ya mazungumzo kufanya uratibu na wengine, au iwapo wanastahili kuendelea kutoa uungaji mkono kwa muungano huo dhidi ya IS.

Marekani imekuwa ikiishutumu Ujerumani kwa kutumia pesa kidogo kwa ulinzi

"Wacha nisisitize mambo kadhaa yanayohusiana na suala hilo. Kwanza iwapo NATO itajiunga na muungano huo, jambo hilo halitobadili jukumu la NATO," alisema Stoltenberg, "kwasababu NATO itaendelea kuunga mkono, itaendelea kuelekeza nadhari yake katika kutoa mafunzo. NATO haitohusika katika operesheni za kijeshi."

Jens StoltenbergPicha: DW/Z. Ljubas

Merkel pia alisema kwamba ameweka wazi kwa Stoltenberg kwamba Ujerumani haiko tayari kuongeza jukumu lake katika vita vya ulimwengu mzima dhidi ya IS, hata iwapo NATO italikubali ombi la Marekani, kwa muungano huo kuchukua jukumu rasmi katika muungano unaopambana na IS.

Stoltenberg pia alizungumzia mzozo wa muda mrefu uliopo baina ya Ujerumani na Marekani kuhusiana na matumzi ya pesa katika ulinzi. Amesema wanachama wa NATO walikuwa hawakukubaliana kutumia asilimia mbili ya mapato ya nchi zao kwa ulinzi, bali kusitisha kushuka kwa utumizi wa pesa kwa jeshi na kuelekea katika lile lengo lao la asilimia mbili.

Rais Donald Trump ameishutumu Ujerumani kwa kutotumia kiasi kikubwa cha pesa katika ulinzi wake mwenyewe.

Mwandishi: Jacob Safari/APE/Reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga