Kansela Merz:Ujerumani haitarejea kwenye nishati ya nyuklia
12 Machi 2026
Katika mkutano wa kilele kuhusu nishati ya nyuklia karibu na Paris mapema wiki hii, Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen alielezea mpito kutoka nishati ya nyuklia uliofanywa na baadhi ya nchi za EU kama "kosa la kimkakati.” Alisema nishati ya nyuklia ni "chanzo cha kuaminika, chenye gharama nafuu cha umeme wenye uzalishaji mdogo wa hewa chafu.” Alitangaza pia msaada mpya wa kifedha wa EU kwa mitambo ya nishati ya nyuklia.
Maneno ya von der Leyen yalisikika sana nchini Ujerumani, ambayo ilizima kinu chake cha mwisho cha nyuklia mwaka 2023.
Baba yake von der Leyen, Ernst Albrecht, kama binti yake mwanachama wa chama cha kihafidhina cha Christian Democratic Union (CDU), alikuwa mkuu wa serikali ya jimbo la Lower Saxony katika miaka ya 1970 na mfuasi mkubwa wa nishati ya nyuklia.
Hata hivyo alishindwa katika jaribio lake la kuanzisha hifadhi ya mwisho ya taka zenye mionzi mikali mashariki mwa jimbo lake. Kijiji cha Gorleben, ambacho kilichaguliwa kama eneo la kujenga hifadhi hiyo, kiligeuka kuwa ishara ya mapambano ya mamia ya maelfu ya watu dhidi ya nishati ya nyuklia. Hifadhi hiyo haikujengwa kamwe.
Hakuna mitambo ya nyuklia nchini Ujerumani tangu 2023
Wito wa von der Leyen wa kurejea kwenye nishati ya nyuklia unapokelewa kwa mitazamo mchanganyiko, au hata hasi, mjini Berlin.
Kuanzia mwaka 1961, jumla ya vinu 37 nchini Ujerumani vilikuwa vikitoa hadi asilimia 30 ya umeme wa taifa. Nchi hiyo ilianza kuachana taratibu na nishati ya nyuklia miaka 15 iliyopita kufuatia janga la Fukushima nchini Japani tarehe 11 Machi 2011. Kituo cha mwisho cha nishati ya nyuklia nchini Ujerumani kilizimwa mwaka 2023. Hispania na Austria pia zimetangaza kuwa zimefunga kabisa mitambo yao ya nyuklia.
Tangu wakati huo, kumekuwa na mjadala wa mara kwa mara nchini Ujerumani kuhusu kama kurejea kwenye nishati ya nyuklia kungekuwa jambo la busara, kutokana na mabadiliko ya uzalishaji wa nishati jadidifu kama jua na upepo, na hasa kutokana na uhaba wa uagizaji wa mafuta na gesi wakati wa migogoro ya kimataifa kama vita vya Ukraine au vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran na kuongezeka kwa mvutano Mashariki ya Kati.
Jumanne, Kansela Friedrich Merz, ambaye pia ni mwanachama wa CDU, alisema serikali zilizopita za shirikisho zilikuwa zimeamua kuachana na nishati ya nyuklia na kwamba kubadilisha uamuzi huo haiwezekani. "Ninajuta hili,” alisema, "lakini ndivyo ilivyo, na sasa tunajikita katika sera ya nishati tuliyonayo.”
Ingawa CDU na chama rafiki cha Christian Social Union (CSU) cha Bavaria vinaunga mkono nishati ya nyuklia, Merz pia anajua kuwa kubadilisha mwelekeo huo kungehitaji kupata wingi wa kura katika Bundestag, bunge la chini la Ujerumani. Na kura za chama cha mrengo mkali wa kulia cha Alternative for Germany (AfD) zingehitajika ili kufikia idadi hiyo. Merz amesema hatashirikiana na AfD.
SPD yakataa mitambo mipya ya nyuklia
Mshirika mdogo wa muungano wa wahafidhina, chama cha mrengo wa kati kushoto cha Social Democratic Party (SPD), kimekataa pendekezo la von der Leyen la kurejea kwenye nishati ya nyuklia. Waziri wa Mazingira Carsten Schneider wa SPD alisema nishati ya nyuklia tayari imewagharimu walipa kodi mabilioni ya fedha. "Iwapo teknolojia yenye hatari bado inategemea msaada wa serikali baada ya karibu miaka 75, na mbadala bora tayari zipo kwa muda mrefu, basi hatua zinapaswa kuchukuliwa,” alisema.
Schneider pia alikataa wazo la kuzingatia zaidi vinu vidogo vinavyohamishika, vinavyojulikana kama Small Modular Reactors (SMRs). "Mitambo hii midogo ya nyuklia imekuwa ikiendelezwa kwa miongo kadhaa, lakini bado hakuna mafanikio makubwa, na bado kuna changamoto ya kupata ruzuku,” alisema.
Markus Krebber, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni kubwa zaidi ya umeme nchini Ujerumani, RWE, hivi karibuni alikataa wazo la vinu vidogo. "Kwa hali ilivyo sasa, uwekezaji katika SMRs hauwezekani kwa kampuni binafsi,” Krebber aliiambia tovuti ya habari ya Político. Alisema hakuna msambazaji duniani anayeweza kuahidi muda wa ujenzi kwa gharama zilizokubaliwa na zilizowekwa mapema. Kampuni hazitatoa ufadhili kwa vinu vidogo, alisema.
Ufaransa yaongoza muungano wa nyuklia wa nchi 15 za EU
Nchi nyingi za EU zinazingatia kupanua nishati ya nyuklia. Ufaransa inaendesha vinu 57 na imeunda kundi la nchi 15 za EU zinazotetea kujengwa kwa mitambo mipya ya nyuklia. Kundi hilo linajumuisha nchi kama Sweden na Italia.
Nchini Ujerumani, janga la Chernobyl mwaka 1986 lilisababisha kufikiriwa upya kwa nishati ya nyuklia. Chama cha Greens, kilichoanzishwa Ujerumani Magharibi mwaka 1980, kilifanya kampeni kubwa dhidi ya nishati ya nyuklia. Baada ya kuingia serikalini pamoja na SPD, walifanikiwa kusukuma sera ya kuachana nayo taratibu mwaka 2000.
Hata hivyo sera hiyo ilibadilishwa wahafidhina waliporejea madarakani katika muungano na chama cha kiliberali cha Free Democrats (FDP), na mwaka 2010 wakaamua kuongeza muda wa uendeshaji wa vinu vya nyuklia nchini Ujerumani.
Lakini hali ilibadilika tena: Kufuatia tetemeko la ardhi na tsunami, ajali kubwa ya kuyeyuka kwa vinu ("super meltdown”) ilitokea katika kituo cha nyuklia cha Fukushima nchini Japani mwaka 2011. Kansela Angela Merkel mwenyewe alisimamia kurejea kwa mkakati wa kuachana na nishati ya nyuklia. Na uamuzi huo bado upo hadi leo.