Ujerumani haitashiriki vita Syria
12 Aprili 2018Rais wa Marekani Donald Trump amesema kwamba shambulio dhidi ya Syria huenda likafanyika "hivi karibuni ama hata sio hivi karibuni kabisaa" akidai kwamba hajawahi kuashiria muda wa kujibu shambulio hilo la gesi ya sumu , suala aliloonesha ishara kwamba lingefanyika hivi karibuni.
Kansela wa Ujerumani amesema ," tunapaswa kukiri kwamba ni dhahiri hatua za kuharibu silaha hizo za sumu haikufanyika kwa ukamilifu," alisema , sio kwamba hakuna ushahidi wa kutosha kwamba serikali ya Syria ilitumia silaha hizo za sumu. Serikali ya Syria iliepuka mashambulizi ya Marekani na Ufaransa mwaka 2013 katika kujibu shambulio linaloshukiwa kuwa ni la gesi ya sarin kwa kukubali kukabidhi hazina yake ya silaha za sumu.
Kufuatia madai ya matumizi ya gesi ya sumu katika eneo lililokuwa linashikiliwa na waasi la Douma, rais wa Marekani Donald Trump wiki hii aliongeza mbinyo dhidi ya Damascus , akionya katika maandishi yake kadhaa katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba "makombora yanakuja" ili kulipiza kisasi. Msemaji wa serikali ya Urusi Dmitry Peskov hata hivyo amesema Urusi inafuatia kwa karibu taarifa zinazotoka Marekani.
"Urusi inafuatilia kwa karibu matamshi kutoka Marekani na bado tunaamini kwamba ni muhimu sana kuepuka hatua zozote ambazo zitaweza kusababisha msuguano nchini Syria. Tunafikiri hali hiyo italeta athari mbaya katika mchakato mzima wa utulivu wa Syria."
Ujerumani haitashiriki vita
Kansela wa Ujerumani angela Merkel amesema "hatua kadhaa " zitatiliwa maanani kujibu shambulio hilo la gesi ya sumu, lakini aliondoa uwezekano wa hatua za kijeshi. Ujerumani haitashiriki kijeshi, lakini itatoa msaada iwapo wawakilishi katika baraza la Usalama la Umoja wa mataifa , wataamua kuchukua hatua mbali na hatua za kidiplomasia" alisisitiza.
Ufaransa lakini inatarajiwa kujiunga na Marekani na Uingereza kufanya mashambulio ya anga ama njia nyingine za mashambulio kujibu shambulio hilo la silaha za sumu , lakini inabaki bila uhakika iwapo hilo huenda likatokea ama hata iwapo kweli litatokea.
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema leo kwamba nchi yake inaushahidi kwamba serikali ya Syria ilifanya shambulio hilo la silaha za sumu wiki iliyopita na itaamua iwapo ishambulie wakati taarifa zote muhimu litakapokuwa zimekusanywa.
"kuna mfumo wa sheria za kimataifa, tuna ushahidi kwamba wiki iliyopita shambulio la gesi ya sumu ya klorine lilifanyika na kwamba lilifanywa na serikali ya Bashar al-Assad. Sheria za kiutu na kutoa nafasi kwa misaada ya kiutu, kusaidia asasi zisizo za kiserikali kuwasaidia watu ndani ya nchi hiyo, katika njia kwenda Idlib na kuwatoa raia kutoka katika eneo hilo. Watoto pamoja na wanawake. Ili kutoona tena picha za kutisha za uhalifu ambapo tuliona watoto na wanawake wakifariki kutokana na kushindwa kupumua."
Rais wa Marekani Donald Trump ameandika katika ukurasa wa Twitter leo asubuhi, "Sijasema lini shmabulio dhidi ya Syria litafanyika. Huenda ni hivi karubuni ama hata pengine sio hivi karibuni kabisa !" wakati huo huo meli za kijeshi za Urusi zimeondoka kutoka katika vituo vyake katika bahari ya Mediterania kwa kile kilichoelezwa kuwa ni usalama wake, hali iliyoelezwa na makamu mwenyekiti wa kamati ya ulinzi ya Urusi kwamba ni hatua za kawaida , wakati kuna kitisho cha shambulio.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe
Mhariri: Iddi Ssessanga