1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani haitishwi na Marekani kuondoa wanajeshi

23 Julai 2020

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Annegret Kramp-Karrenbauer ameashiria kwamba kitisho kilichotolewa na Marekani mwezi uliopita cha kuwaondoa wanajeshi wake nchini humo hakutaathiri ushirikiano baina yao.

Berlin I Kramp-Karrenbauer stellt "Dein Jahr für Deutschland" vor
Picha: Getty Images/S. Gallup

Kramp Karrenbauer amesema kitisho hicho hakitaathiri mahusiano kati ya mataifa hayo mawili, ingawa mpango huo unauweka mashakani ushirikiano katika Jumuiya ya Kujihami ya NATO. 

"Iwapo wanajeshi hao watasalia Ulaya, basi hilo litabakia kama jukumu la Marekani kuelekea NATO. Lakini iwapo watahamishiwa kwenye kituo kingine katika ukanda wa bahari ya Hindi na Pasifiki, ni wazi hatua hiyo itaashiria mabadiliko ya mkakati wa Marekani, hatua ambayo itaibua mjadala ndani ya NATO", amesema waziri huyo wa ulinzi alipozungumza na DW mapema hii leo.

Mwezi uliopita, rais wa Marekani Donald Trump aliidhinisha kuondolewa kwa zaidi ya robo ya wanajeshi wa nchi yake walioko Ujerumani, akisema hatua hiyo itasaidia kuimarisha usalama barani Ulaya.

Rais Donald Trump wa Marekani imetishia kuwaondoa wanajeshi wake Ujerumani kwa kuwa Ujerumani imeshindwa kufikia lengo la mchango wake kwa NATO.Picha: Reuters/L. Millis

Kabla ya tangazo hilo la mwezi Juni, serikali ya Trump iliiomba Ujerumani kuongeza mchango wake kwenye bajeti ya ulinzi ili kufikia lengo la mchango wake kwenye jumuiya hiyo ya NATO la asilimia 2 ya pato lake jumla la ndani. Trump alionya iwapo watashindwa kufanya hivyo angeondoa wanajeshi karibu 10,000 kati ya 34,500 waliopo nchini Ujerumani, kama adhabu ya kushindwa kufikia lengo la mchango wake.

Mataifa wanachama wa NATOMkutano wa NATO wazongwa na mivutano walikubaliana kuongeza michango kwenye bajeti ya ulinzi na kufikia asilimia 2 ya mapato yao ya ndani hadi ifikapo mwaka 2024. Ujerumani hadi sasa hado haijafikia lengo hilo. Kramp-Karrenbauer aliwahi kusema haitoshi kuangazia tu pato la ndani katika mchango wa taifa kwenye bajeti hiyo ya ulinzi na uwajibikaji kwenye muungano huo wa kijeshi.

Mradi wa Nord Stream 2 ambao Marekani inaupinga vikaliPicha: DW

Kuhusiana na mradi wa bomba la kusafirisha gesi la Nord Stream 2 linalopingwa vikali na Marekani, Kramp-Karrenbauer ameunga mkono miito ya mazungumzo kuhusiana na mradi huo, lakini akionya kwamba kitisho cha vikwazo kilichotolewa na Marekani huenda kikawa kinyume na sheria za kimataifa. Amesema linapokuja suala la vitisho vya Marekani, serikali ya Ujerumani huwa na msimamo ulio wazi kwamba vitisho hivyo haviendani na sheria za kimataifa.

Marekani imekuwa ikiupinga mradi wa bomba hilo litakalosafirisha gesi asilia kutoka Urusi kupitia bahari ya Baltiki hadi Ujerumani, huku Trump wiki iliyopita akiyaonya makampuni yanayojihusisha na mradi huo kwamba yatakabiliwa na adhabu iwapo hayataachana nao. Kulingana na Washington pamoja na mataifa kadhaa ya Ulaya mashariki, mradi huo utaongeza utegemezi wa Umoja wa Ulaya kwenye nishati ya Urusi.

Hata hivyo, Ujerumani imeionya Marekani kutoweka vikwazo hivyo na badala yake ifanye majadiliano na washirika wake, suala ambalo Kramp-Karrenbauer amelirudia tena.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Mike Pompeo ameelekea Denmark hapo jana na suala ya mradi ya bomba hilo linatarajiwa kuwa moja ya ajenda kwenye mazungumzo yake na waziri mkuu Mette Frederiksen na waziri wa mambo ya kigeni Jeppe Kofod. Denmark, iliruhusu bomba hilo kupitishwa kwenye eneo lake.

Mashirika: DW