Ujerumani ilivyopokea ushindi wa Trump
9 Novemba 2016Kansela huyo pia alimkubusha rais huyo mteule wajibu alionao duniani baada ya kupigiwa kura kwa wingi na Wamarekani.Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Berlin pindi baada ya John Donald Trump kutangazwa mshindi kansela Merkel alianza kwa kusema hivi “Nampongeza mshindi wa uchaguzi wa urais nchini Marekani Donald Trump. Marekani ni taifa linaloheshimika na linalozingatia democrasia tangu zamani. Kampeini ya mwaka huu ilikuwa ya aiana yake, na wakati mwingine ilikumbwa na makabiliano yaliyokuwa magumu kuvumiliwa.” Kansela Merkel amesema yuko tayari kwa ushirikiano wa karibu na rais huyo mteule chini ya misingi ya maadili ya mataifa yanayopakana na bahari ya Atlantic.Wakati wa mkutano huo Merkel alisisitiza kuhusu uhusiano wa karibu wa kihistoria kati ya Ujerumani na Marekani. Hata hivyo alimtaka Trump kuelewa anakabiliwa na kibarua kigumu kutokana na Marekani kuwa taifa lenye uwezo mkubwa duniani linapokuja swala la kiuchumi na hata nguvu za kijeshi.
Wakati wa kampeini zake Trump alimtuhumu Merkel kutokana na kile alichokisema ni kuangamiza Ujerumani kutokana na sera yake ya milango wazi kwa wakimbizi, lakini baadae alimtaja kuwa kiongozi anaye heshimika duniani. Nae waziri wa mambo ya nje Frank-Walter Steinmeier ameonya sera za kigeni za Marekani huenda zisiweze kutabirika baada ya Trump; kuchaguliwa kwa wingi wa kura nchini Marekani. Steinmeier amesema anahofia hali hiyo huenda ikayafanya mambo kuwa magumu zaidi.“Wengi wetu tunatumai hakutakuwepo na mabadiliko makubwa ya sera za kigeni. Donald Trump alizungumzia hilo kwa kina wakati wa kampeini zake,sio tu kuhusu bara ulaya lakini pia kuhusu Ujerumani.Nadhani itatubidi katika siku za usoni kuzoea sera za kigeni za Marekani zisizotabirika, na lazima pia tukubali kuwa Marekani itafanya maamuzi kivyake.”
Donald Trump anataka kuijadili upya mikataba ya kibiashara ya Marekani ili kupunguza nakisi za biashara. Kwa mujibu wa Steinmeier,rais huyo mteule pia amechukua msimamo utakaohatarisha uhusinao kati taifa hilo na washirika wake wa karibu bara Ulaya ,Asia na mashariki ya kati. Wakati wa kampeini zake Trump aliahidi kuanzisha uhusiano mzuri na Urusi, ambao ulivurugika chini ya utawala wa rais Barack Obama ,baada ya rais wa Urusi Vladmir Putin kuingilia vita vya Syria na vile vya Ukraine eneo la Krimea.
Mwandishi:Jane Nyingi/AFPE/AP
Mhariri:Yusuf Saumu