1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Ujerumani imeionya Israel dhidi ya hukumu ya kifo

28 Februari 2023

Ujerumani imeionya Israel kuwa litakuwa kosa kubwa kuanzisha adhabu ya kifo kwa wanaopatikana na hatia ya kuwauwa raia wa Israel. Hii ni baada ya kamati ya mawaziri kuunga mkono pendekezo hilo.

COP27 I Annalena Baerbock
Picha: Christophe Gateau/dpa/picture alliance

 

Waziri wa Mambo ya Kigeni Annalena Baerbock, baada ya mazungumzo na mwenzake wa Israel Eli Cohen mjini Berlin, amesema Ujerumani ina wasiwasi mkubwa kuhusu mpango wa kuanzisha adhabu ya kifo. Amesema katika kikao cha waandishi habari pamoja na Cohen kuwa Ujerumani inapinga vikali adhabu ya kifo, na italiibua suala hilo kote ulimwenguni.

Jumapili iliyopita, kamati ya mawaziri ya Israel inayohusika na masuala ya sheria iliunga mkono mswada utakaoidhinisha adhabu ya kifo, ambao ulikuwa sehemu ya makubaliano ya muungano uliofikiwa kati ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na mshirika wake wa kisiasa wa mrengo mkali wa kulia.