Covid-19 huenda ikazidisha kudorora kwa hali ya kibinadamu
4 Agosti 2020Wakati huo huo, wataalamu na wanadiplomasia wa Umoja wa Mataifa wanaonya kuwa janga la Covid-19 huenda likazidi kuzorotesha hali ya kibinadamu katika sehemu zinazoshuhudia mapigano duniani.
Mkuu wa muungano wa madaktari hapa Ujerumani Susanne Johna amesema katika mahojiano yaliyochapishwa kwenye gazeti la Augsburger Allgemeine leo Jumanne kuwa Ujerumani tayari inakabaliwa na wimbi la pili la maambukizi ya virusi vya Corona.
Mkuu huyo wa muungano wa madaktari ameyasema hayo wakati idadi ya maambukizi ya virusi vya Corona ikizidi kuongezeka katika wiki za hivi karibuni huku wataalamu wa afya wakionya kuwa watu kupuuza agizo la kutokaribiana na kudumisha usafi kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia kuenea kwa kasi kwa virusi hivyo.
Susanne ameonya kuwa watu kutamani hali kurudi kama kawaida huenda ikavuruga mafanikio iliyopata Ujerumani katika kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo.
Ametoa wito kwa watu kuendelea kufuata maagizo ya afya kama vile kukaa umbali wa angalau mita mbili baina ya mtu na mtu na pia watu kuendelea kuvaa barakoa.
Kwa mujibu wa taasisi ya afya ya Robert Koch, idadi ya maambukizi ya virusi vya Corona hapa Ujerumani imeongezeka kwa 879 hadi 211,281 kufikia leo Jumanne. Vile vile, watu 9,156 wamefariki dunia kutokana na ugonjwa huo unaoathiri zaidi mapafu.
Janga la Covid-19 linadhoofisha mipango ya kupeleka misaada katika sehemu za mizozo
Wakati hayo yakiarifiwa, wataalamu na wanadiplomasia wa Umoja wa Mataifa wanaonya kuwa janga la Covid-19 huenda likazidi kuzorotesha hali ya kibinadamu katika sehemu zinazoshuhudia machafuko na pia kutishia kuathiri uchumi.
Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa Richard Gowan amesema janga la Covid-19 linadhoofisha mipango ya kupeleka misaada katika sehemu zinazoshuhudia mapigano duniani.
Mtaalamu huyo ameliambia shirika la habari la AFP kuwa hali hiyo huenda ikawa na athari kubwa ya kiuchumi na hivyo basi kuongeza mzozo zaidi.
Kauli yake inajiri baada ya wito uliotolewa na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres mnamo mwezi Machi wa kutaka pande zinazohasimiana katika mataifa kama vile Yemen, Libya na Syria kusitisha mapigano kupuuzwa.
Juu ya hayo, vizuizi na marufuku ya kuingia na kutoka iliyowekwa katika nchi nyingi ili kuzuia kusambaa kwa virusi vya Corona imezuia safari za wajumbe, vikosi vya kulinda amani pamoja na mashirika yasiokuwa na kiserikali kusambaza misaada ya kibinadamu kwa raia wanaokabiliwa na ghasia na machafuko nchini mwao.
Chanzo AFP/Reuters/