Ujerumani itaupunguza mafao ya wakimbizi?
8 Novemba 2023Karibu wakimbizi 200 huwasili mjini Berlin kila siku. Wanastahili kuishi kwa muda mfupi katika kituo cha kwanza cha mapokezi kama kilichokuwa katika uwanja wa zamani wa Tegel mjini Berlin kabla kuhamishiwa katika makaazi mengine mjini humo.
Ila kuna uhaba wa kupata nyumba za makaazina baadhi ya wakimbizi wamekwama katika kituo hicho cha Tegel kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Kwa sasa watu elfu 4 wanaishi katika kituo hicho kinachotarajiwa kupanuliwa ili kiweze kuwa makaazi ya watu elfu 8.
Hali ya wakimbizi ilivyo katika mji huo mkuu wa Ujerumani ndivyo ilivyo katika miji na serikali zengine za mitaa kote Ujerumani.
Soma pia:Ujerumani yaridhia masharti magumu kwa wahamiaji na wakimbizi
Mwaka huu pekee, wahamiaji 220,000 wametuma maombo yao ya awali ya kuomba hifadhi.
Kando na hayo, kuna wakimbizi milioni moja wanaotokana na vita vya Urusi na Ukraine, wao nao wanajisajili katika mamlaka za Ujerumani ili wapewe makaazi na serikali.
Kote Ujerumani, mameya na wakuu wa wilaya wanasema hawajui watawapa vipi hifadhi wakimbizi wanaopewa na serikali kutokana na mfumo wa ugavi ulioko.
Suala la ukosefu wa makaazi ni moja tu ila kuna ukosefu wa wafanyakazi wa usimamizi pia na uhaba wa nafasi katika chekechea na shule na huduma za ushauri nasaha kwa wakimbizi wanaokabiliwa na hali ya uoga wa kupitiliza.
Lazima kuwe na ukomo wa idadi ya wahamiaji
Utafiti uliofanywa na shirika moja la huduma za habari kuhusiana na masuala ya kuwaleta watu pamoja unaonyesha kwamba watu waliohusishwa katika utafiti huo wanapendekeza, kuwekwa ukomo wa uhamiaji ili kuhakikisha kwamba watu wachache au hakuna watu wanaotumwa katika serikali zao za mitaa, kwasababu hakuna uwezo tena wa kuwahudumia.
Wanatoa wito pia wa kupewa fedha zaidi na serikali ya shirikisho na hakikisho la fedha hizo kutolewa kwa muda mrefu zaidi.
Katika utafiti huo, ni watu wachache pekee waliosema kwamba wangependelea kuona wakimbizi wakirudishwa makwao.
Soma pia:Ujerumani kuweka masharti magumu ili kuzuia uhamiaji
Kwa sasa ni maombi ya uhamiaji ya karibu watu 250,000 yaliyokataliwa Ujerumani. Katika visa vingine mamlaka hata hazifahamu walipo baadhi ya watu.
Na watu wengine 200,000 hawawezi kurudishwa walikotoka kwa kuwa ama hakuna nchi inayoweza kuwachukua au nchi wanayotokea inakabiliwa na vita au wana magonjwa makubwa ambayo hayawezi kutibiwa katika nchi wanazotokea.
Wahamiaji ambao maombi yao yamekataliwa
Mnamo mwezi Oktoba, serikali ya Ujerumani iliwasilisha muswada wa kuongeza idadi ya wakimbizi wanaorudishwa makwao ila idadi ya wakimbizi katika miji mingi kwa sasa inajumuisha wahamiaji wapya.
Wanasiasa wa Ujerumani pia wanajadili kuhusu suala la mafao ya kijamii wanayopewa wakimbizi, ambayo nchini Ujerumani yanaonekana kuwa mazuri zaidi kuliko katika nchi nyingine yoyote ya Umoja wa Ulaya.
Wanasiasa wa Kihafidhina wanaelezea suala hili kama kivutio cha wahamiaji Ujerumani na wamependekeza wakimbizi wanaowasili wapunguziwe hela wanazopewa au wasipewe chochote kabisa.
Soma pia:Uhamiaji: Ujerumani yajipanga kushughulikia masuala ya wakimbizi
Lakini watafiti wamekosoa hatua hiyo wakisema ni hatua iliyojaribiwa katika miaka ya tisini na tena mwaka 2015 ila haikufanikiwa.
Wakimbizi ambao ni watu wazima wanaoishi katika vituo vya mapokezi Ujerumani, kwa kawaida wanapewa makaazi na juu yake wanapewa yuro 150 za matumizi kila mwezi.
Fedha hizo zipo kisheria na mahakama ya katiba iliamua kwamba fedha hizo haziwezi kupunguzwa.