Ujerumani inatakiwa iwajibike zaidi barani Afrika
4 Desemba 2012►Wakati mizozo ikiendelea kulitafuna bara la Afrika, suali linalojitokeza ni ikiwa mataifa dhaifu yaliyo kwenye migogoro yanahitaji kushughulikiwa kwa aina mpya na jumuiya ya kimataifa. Na je ni namna gani taifa kama Ujerumani linawajibika katika kuimarisha siasa ya maendeleo katika nchi mfano wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Mali?
Mizozo katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo na Mali inaweza kuenea katika maeneo mbali mbali ya Afrika na nje ya bara hilo.Sababu ni tofauti: Katika nchi tajiri kwa mali ghafi, Kongo, serikali haijui chochote kinachotokea katika eneo la mizozo la mashariki.Wakaazi wa eneo hilo hawawezi kutegemea si ulinzi wa polisi wala huduma kutoka idara za serikali.Hata miundo mbinu ya usafiri hakuna katika nchi hiyo ya pili kwa ukubwa barani Afrika.
Hata baada ya uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasi uliodhaminiwa na nchi za Ulaya mwaka 2006,hakuna huduma zozote za serikali katika eneo hilo.Badala yake ,matumizi ya nguvu yaliyosababishwa na miongo kadhaa ya vita ndiyo yanayoshuhudiwa.Kutokana na mchanganyiko wa kikabila pamoja na mataifa jirani pamoja pia na utajiri ulioko chini ya ardhi,mzozo wa Kongo unaweza kusababisha vurugu katika eneo lote la Afrika Mashariki.Hali hiyo isingekuwa mpya kwasababu imeshawahi kushuhudiwa katika miaka ya 90 pale majeshi kutoka nchi nane yalipopigana vita vilivyokuwa vikijulikana kama "vita vya Afrika"-watu milioni nane walipoteza maisha yao wakati ule.
Nchini Mali pia akrabu za saa zinarejea nyuma:wapiganaji wa itikadi kali ya dini ya kiislam na makundi ya waasi wamewatia katika hali ya hamu na ghamu wakaazi wa nchi hiyo ya Sahel ambao hadi hivi karibuni walikuwa wakifuata imani ya wastani ya dini ya kiislam.
Hatari kutoka Mali inaweza kuenea hadsi Ulaya,wadadisi wanasema.
Kitisho hicho bado hakijawaingia sana wajerumani,anahisi mwakilishi wa kansela Angela Merkel anaeshughulikia masuala ya bara la Afrika Günter Nooke.Anahisi hata hivyo wakati umewadia kutilia maanani pia uwezekano huo."Tunabidi tujifunze kuanzisha mijadala kuhusu siasa ya nje,sera za kijeshi,sera za usalama,haki za binaadam na misaada ya maendeleo" anasisitiza bwana Günter Nooke.
Msemaji wa chama cha upinzani cha walinzi wa mazingira anaeshughulikia siasa ya maendeleo bibi Ute Koczy anashadidia umuhimu wa kuwajibika zaidi Ujerumani barani Afrika.Anasema cha muhimu ni kuhakikisha namna ya kuimarisha juhudi hizo.
Suala la misaada ya maendeleo halipiti njia nyengine isipokuwa ile ya serikali anasema bibi Ute Koczy na kuendelea:"Hatuna njia nyengine nyengine isipokuwa kutegemea serikali,na kimsingi ni serikali zinazochaguliwa na wananchi.Nchi mfano wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani inalazimika kushirikiana na serikali na ndio maana nionaonvyo mie tunabidi tunabidi tuzungumze kinaga ubaga."
Msimu wa kiangazi uliopita serikali kuu ya Ujerumani imebuni mkakati maalum wa jinsi ya kuyashughulikia mataifa dhaifu..Siku za mbele,patahitajika kuwepo uwiano katika kuyashughulikia masuala ya siasa ya nje,usalama na misaada ya maendeleo katika nchi kama hizo.
Mwandishi: Schaeffer, Ute/Hamidou Oummilkheir
Mhariri: Mohammed Khelef