1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani inaweza kumshtaki Assad kwa uhalifu wa kivita

27 Novemba 2020

Waendesha mashtaka wa serikali ya shirikisho ya Ujerumani wanachunguza ushahidi wa matumizi ya kemikali katika vita vya Syria.

Syrien Ein Schatten fällt auf die Fahne mit dem Portait von Präsident Bashar Assad
Picha: Muzaffar Salman/AP Photo/picture-alliance

DW na gazeti la Der Spiegel walifanikiwa kuwahoji mashahidi pamoja na kupata nyaraka muhimu ambazo ni sehemu ya uchunguzi huo wa kihistoria.

Agosti 21, 2013 makombora yaliyokuwa na sumu ya sarin yalishambulia mashariki mwa Ghouta. Eman F., muuguzi mmoja anasema ''siku hiyo ilikuwa kama ya hukumu'', kana kwamba watu walikuwa mchwa na waliouawa na dawa ya wadudu.

Takriban watu 1,000 waliuawa

Eman ameiambia DW kwamba watu wengi waliuawa barabarani, magari yalisimama, watu walijazana ndani ya magari ambapo wengine walikufa wakati wakijaribu kukimbia. Kwa mujibu wa vyanzo kadhaa vinavyojitegemea, takriban watu 1,000 waliuawa katika shambulizi hilo, wakiwemo zaidi ya watoto 400.

Lakini hili linatosha kwa waendesha mashtaka wa Ujerumani kufungua mashtaka? Kwa wataalamu wa sheria za kimataifa, moshi wa bunduki hauhitajiki kufungua mashtaka kwa kiwango hiki.

Eman na mumewe Mohammed walishuhudia shambulizi la sumu ya sarin GhoutaPicha: Birgitta Schülke/DW

Robert Heinsch, mkurugenzi wa Jukwaa la Kalshoven-Gieskes linaloshughulika na Sheria ya Binaadamu ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Leiden, anasema kwa kuwa uhalifu wa kivita mara nyingi hufanywa katika mfumo wa vikosi vya kijeshi, sheria za kimataifa zinatambua kuwa makamanda wanaotoa amri wanawezesha ukiukaji kama huo.

"Watu wanaotoa amri kwa wanajeshi wa kawaida au yeyote anayehusika kwa kufanya mashambulizi, anaweza kushtakiwa kwa sababu ya vitendo vyake vya kuamuru. Au hata kama mtu hakuamuru mwenyewe, lakini alikuwa anafahamu au alipaswa kujua kuhusu mashambulizi. Kwa sababu ya kazi zao kama makamanda wa jeshi, wanaweza kuwajibika," alifafanua Heinsch.

Soma zaidi: Gesi ya Sarin ilitumika kama silaha ya kemikali Syria 

Aidha, Steve Kostas, afisa wa ngazi ya juu wa sheria katika Taasisi ya Haki ya Jamii anasema kuwa wana ushahidi kwamba Rais Bashar al-Assad anahusika katika kufanya uamuzi.

"Siwezi kusema kwamba sisi wenyewe tumethibitisha hilo, lakini hakika tuna taarifa zinazoonesha kuhusika kwake katika mashambulizi ya sumu ya sarin," alisema Kostas.

Mabaki ya roketi iliyotumika kuushambulia mji wa Ghouta, SyriaPicha: Getty Images/AFP/H. Mohamed

Kostas anabainisha kuwa wameonesha kwamba kulikuwa na kitengo maalum kinachoitwa Tawi 450 ambacho kilihusika sana kupanga na kutekeleza mashambulizi ya sumu ya sarin. Anasema wameonesha orodha ya makamanda wanaohusika katika kitengo hicho na uhusiano wake na ikulu ya rais.

Nchini Ujerumani, sheria ya kuwashtaki wahalifu bila kujali uhalifu huo ulipofanyika, imetumika tu mara moja kumshtaki mhalifu. Mwaka 2015, majaji wa Ujerumani walimkuta na hatia kiongozi wa waasi wa Rwanda, Ignace Murwanashyaka pamoja na msaidizi wake kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu.

Hukumu ya Murwanashyaka ilibatilishwa miaka mitatu baadae na alifariki dunia wakati anasubiri kesi yake isikilizwe tena.

Kesi nyingine pekee ambayo ilitumia sheria ya kuwashtaki wahalifu bila kujali uhalifu huo ulipotendeka, ni kesi katika mji wa Koblenz nchini Ujerumani iliyowalenga maafisa wa utawala wa Syria kwa madai ya kutumia mfumo wa utesaji.

(DW)

 

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW