1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani itaipa Ukraine msaada wa kijeshi euro bilioni 2.7

Angela Mdungu
13 Mei 2023

Serikali ya Ujerumani imesema Jumamosi kuwa itaipatia Ukraine msaada mpya wa kijeshi wenye thamani ya zaidi ya euro bilioni 2.7. Msaada huo unajumuisha vifaru vya kivita, mfumo wa ulinzi wa anga pamoja na mabomu.

Deutschland Waffen für die Ukraine
Picha: Martin Meissner/AP Photo/picture alliance

Kauli ya Ujerumani imetolewa wakati nchi hiyo ikijiandaa kwa ujio wa kwanza wa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky tangu Urusi ilipoivamia kijeshi nchi yake mwaka uliopita.

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius, amesema wanataka kuonesha kuwa nchi hiyo inamaanisha kuiunga mkono kwa dhati Ukraine kwa kuipatia silaha zake za kisasa zaidi. Licha ya kwamba ziara ya Zelensky inayotarajiwa kufanyika Jumapili nchini Ujerumani haijathibitishwa rasmi, inatafsiriwa kuwa ishara ya kuimarika kwa uhusiano wa mataifa hayo mawili.

Kwa muda mrefu, Kyiv ilikuwa ikitilia shaka utegemezi wa Ujerumani kwa nishati ya Urusi pamoja na uungaji wake mkono bomba la gesi la Nord Stream uliokuwa ukitetewa na Kansela wa zamani Angela Merkel. Kansela wa sasa, Olaf Scholz, alikubali kuanza kupunguza uingizaji wa nishati ya Urusi baada ya nchi hiyo kuivamia Ukraine. Awali Scholz alisita kuipatia Ukraine silaha kwa kuhofia kuitumbukiza Ujerumani kwenye mzozo.

Msaada mpya wa kijeshi ambao Ujerumani imeipatia Ukraine ni pamoja na vifaru 30, chapa Leopard-1, magari 20 ya kivita chapa ya Marder, zaidi ya magari ya 100 yatakayotumika kijeshi, vifaa vya kujilinda, mifumo ya ulinzi wa anga na ndege 200 zisizo na rubani.

Msaada ulioahidiwa ufikishwe haraka Ukraine

Wakati huo huo, waziri wa mambo ya kigeni wa Ukraine, Dmytro Kuleba ameiomba Ujerumani kuharakisha upelekaji wa msaada mpya iliyoahidi kuipatia nchi yake. Kuleba ameyasema hayo nchini Sweden akiwa katika mkutano na wenzake wa mataifa ya Umoja wa Ulaya. Ameongeza kuwa anafurahi kama juhudi zote zitafanyika ili kuhakikisha misaada hiyo inapelekwa kwa haraka na kwamba ratiba ya kupokea silaha hizo inaweza kujadiliwa.

Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: president.gov.ua

Katika hatua nyingine, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky siku ya Jumamosi aliwasili mjini Rome ambapo atakutana na kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis pamoja na viongozi wengine wa Italia. Zelensky kupitia ukurasa wake wa Twitter muda mfupi baada ya kutua Rome aliandika kuwa ziara yake hiyo ni muhimu kwa ushindi wa Ukraine. Rais Zelensky anaitembelea Italia ambayo ni mwanachama wa Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Kujihami ya NATO, na ni ziara yake ya kwanza nchini Italia tangu Urusi ilipoivamia Ukraine Februari 2022.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW