1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani, Italia na Hispania zakaribia kukata tikiti ya Brazil

7 Septemba 2013

Vigogo vya soka barani Ulaya vyakaribia kukata tikiti fainali za kombe la dunia nchini Brazil.Ghana yaingia katika kundi la timu10 zitakazowania kufuzu kuingia katika fainali za kombe la dunia mwakani nchini Brazil.

Germany's Miroslav Klose (r) and Gyoergy Garics of Austria vie for the ball during the FIFA World Cup 2014 qualification group C soccer match between Germany and Austria at Allianz Arena in Munich, Germany, 06 September 2013. Photo: Tobias Hase/dpa
Mchezo kati ya Ujerumani na AustriaPicha: picture-alliance/dpa

Uhispania , Ujerumani na Italia zimesogea ukingoni mwa kufuzu kukata tikiti ya fainali za kombe la dunia mwakani nchini Brazil huku Cristiano Ronaldo alipachika mabao matatu ya haraka na kuiweka Ureno katika njia kuelekea Brazil ilipopambana na Ireland ya kaskazini.

Safari ya Uholanzi kuelekea katika fainali hizo zitakazofanyika mwakani majira ya joto huko Brazil ilipunguzwa kazi kwa sare dhidi ya timu dhaifu ya Estonia , na Uingereza imepanda juu ya msimamo wa kundi lake kwa ushindi wa kishindo wa mabao 4-0 dhidi ya Moldova.

Ujerumani haikufanya mzaha kabisa jana dhidi ya majirani zao Austria katika azma yao ya kuelekea nchini Brazil mwakani baada ya kuinyoa bila maji kwa mabao 3-0.

Klose na Müller sasa sawa

Katika mchezo ambao ulikuwa ukibadilika badilika kikosi cha kocha Joachim Loew kiliweka mbinyo mkubwa dhidi ya wadogo zao wa Austria na kujisafishia njia kuelekea Brazil mwakani. matukio matatu muhimu ya kukumbukwa yalitokea katika mchezo huo wa jana ambapo mshambuliaji Mroslav Klose amepachika hatimaye bao lake ya 68 akitimiza mabao sawa na mshambuliaji hatari wa Ujerumani , Gerd Mueller ambaye katika enzi zake alipachika mabao 68 katika timu ya taifa.

Miroslav KlosePicha: Patrik Stollarz/AFP/Getty Images

Nahodha wa kikosi cha Ujerumani Philip Lam ameiongoza timu hiyo jana akicheza kwa mara ya 100 katika jezi ya Ujerumani na nahodha wa zamani Michael Balack ameagwa rasimi wakati akiwa kwa mara ya mwisho katika jezi ya Ujerumani katika mchezo huo akiwa katika benchi.

Nahodha wa Ujerumani Philipp LamPicha: picture-alliance/dpa

Kulikuwa na sababu ya kufurahi kwa kikosi kizima cha JoachimLoew kwa kuwa mara kadha Austria imekuwa kikwazo kikubwa kwa Ujerumani katika michezo kama hiyo. Nahodha Philip Lam anadhibitisha hilo.

"Katika mchezo ambao timu unayopambana nayo iko nafasi ya pili katika kundi letu kushinda mabao 3-0 nyumbani ni kitu kizuri sana. Tumeshinda kwa sababu tulifanya juhudi kubwa na hatukutoa nafasi kwa adui kufanya mashambulizi ya hatari, na upande wa mbele tulikuwa wabunifu na tulicheza kama tulivyoelekezwa kufanya".

Ni furaha kubwa

Mshambuliaji wa pembeni Thomas Müller ambaye alipachika bao la tatu katika mchezo huo na kutayarisha la kwanza ambalo liliwekwa wavuni na Miroslav Klose amesema anajisikia vizuri kuwamo katika kikosi hicho cha DFB.

nahodha wa Ujerumani wa sasa Lam kati na nahodha wa zamani Michael Bakack (aliyeshika maua)wakipewa tuzoPicha: picture-alliance/dpa

"Najisikia vizuri sana , kwamba niliweza kusaidia mabao mawili. Goli la Toni lilikuwa muhimu na kiufundi lilikuwa bao safi kabisa. Na tulikuwa na wakati ambapo hatukuweza kwa umaniki kupeleka mpira mbele , kwa kuwa haiwezekani kupeleka mpira kuelekea goli la adui kwa muda wote wa dakika 90 kwa kuwa sisi ni binadamu tu.Lakini , baada ya mabao 3 , Austria haikuwa na fursa ya wazi ya kupata bao. Hatukuwapa nafasi hiyo , kwa jumla tumeridhika".

kocha wa Irelan Giovanni TrappatoniPicha: AP

Sweden inaendelea kuwa mpinzani hatari anayeifuatia Ujerumani katika kundi C . Sweden ilikishinda kikosi cha Ireland cha kocha mkongwe Giovani Trapatoni kwa mabao 2-1. Licha ya kuwa kocha huyo mkongwe anamatumaini bado kuwa kikosi chake kinaweza kukata tikiti kwenda Brazil licha ya matokeo hayo ya kukatisha tamaa. Kocha huyo raia wa Italia amesisitiza kuwa kikosi chake kinahitaji points 4 kutoka mechi mbili. wapinzani wao katika mchezo unaofuata Jumanne ijayo ni Austria na baada ya hapo kikosi hicho cha Trapatoni kinakwaana na Ujerumani.

Kocha wa uingereza Roy HodgsonPicha: AP

Katika usiku uliokiwa na heka heka nyingi , Ubelgiji imerefusha uongozi wake katika kundi A hadi points 5 kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Scotland, Bosnia Herzegovina iliteleza nyumbani dhidi ya Slovakia kwa kuchapwa bao 1-0 , wakati Ugiriki ilikuwa mshindi dhidi ya Liechtenstein na kufungana kileleni mwa kundi G.

Ghasia zimechafua ushindi wa mabo 3-0 wa Romania dhidi ya Hungary na Ukraine imepata ushindi mnono wa mabao 9-0 dhidi ya San Marino katika kundi H. Montenegro ilipoteza kiti chake cha uongozi katika kundi hilo baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Poland na unashikilia usukani pamoja na Uingereza zikiwa zote na points sawa.

Italia imesogea karibu na kukata tikiti yake kwenda Brazil baada ya ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Bulgaria, wakati jamhuri ya Czech imepigwa butwaa baada ya kusalim amri kwa kufungwa mabao 2-1 nyumbani dhidi ya Armenia.

Hodgson ashindwa ampange nani

Kocha wa Uingereza Roy Hodgson amekiri kuwa yuko katika hali ya kuchanganyikiwa kidogo baada ya kocha huyo wa Uingereza kushindwa kufanya uchaguzi katika sehemu ya ushambuliaji licha ya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Moldova jana.

Michael Essien, wa GhanaPicha: dpa

Mshambuliaji wa Manchester United Danny Welberk , alionyeshwa kadi ya njano jana ambayo inamzuwia kucheza katika mchezo dhidi ya Ukraine Jumanne ijayo , timu ambayo iko nyuma ya Uingereza kwa points moja tu. Wayne Rooney na Andy Carroll hawatacheza kwa sababu ni majeruhi na Daniel Sturridge huenda akashindwa kucheza kwa kuwa ana maumivu ya paja, hali hiyo inamuacha Hodgson na chaguo la Rickie Lambert ama Jermain Defoe ambao ndio washambuliaji wake ambao wako fit.

Cristiano Ronaldo ameiokoa Ureno kwa kupachika mabao matatu ya haraka haraka na kuipa timu yake sare muhimu dhidi ya Ireland ya kaskazini, wakati Uholanzi imepoteza points mbili za kwanza katika kinyang'anyiro hiki cha kuwania kufuzu kwenda Brazil kwa kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Estonia.

Lakini Ronaldo hatakuwamo katika kikosi hicho wakati kikatakapocheza mchezo wa kirafiki Jumanne ijayo dhidi ya Brazil mjini Boston kutokana na maumivu.

Ghana yajaribu bahati

Katika bara la Afrika kikosi cha Black Stars ya Ghana , imenyakua moja kati ya nafasi saba zilizobaki katika kinyang'anyiro cha kufuzu kucheza katika fainali za kombe la dunia mwakani nchini Brazil katika kanda ya Afrika , wakati timu hiyo iliyofikia robo fainali mwaka 2010 ikiishinda Zambia kwa mabao 2-1 katika kundi la D.

Serena Williams aingia fainaliPicha: Reuters

Zambia mabingwa wa mataifa ya Afrika mwaka 2012 imeondolewa katika kinyang'anyiro hicho cha kuwania nafasi ya kucheza katika fainali za kombe la dunia.

Wakati Michael Essien akirejea katika kikosi hicho baada ya kukaa nje kwa muda mrefu kutokana na mauamivu, ushindi wa Ghana katika uwanja wa Baba Yara mjini Kumasi unaifanya timu hiyo kujiunga na Cote D'ivoire, Misri na Algeria katika michezo ya mchujo mwezi Oktoba na novemba mwaka huu na kuamua ni timu gani itaingia katika kundi la timu tano kutoka bara la Afrika kucheza kule Brazil mwakani.

Timu nyingine sita zitakazojiunga na timu hizo zitaamuliwa leo(07.09.2013) na kesho Jumapili(08.09.2013). Baadhi ya vigogo vya soka la Afrika , Nigeria , Cameroon, Senegal na Tunisia ni miongoni mwa timu ambazo zitaweza kujiwekea nafasi katika michuano hiyo itakayofanyika nyumbani na ugenini.

Argentina na Colombia hazijaweza kukata tikiti zao jana huenda hadi mchezo ujao baada ya uruguay kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Peru jana.

Chile iliishinda Venezuela kwa mabao 3-0 na kupanda juu hadi nafasi ya tatu katika msimamo wa kundi la America ya kusini, points mbili nyuma ya timu hizo mbili za juu.

Wakati kinyang'anyiro hicho kinachoshirikisha timu 16 kitakapomalizika mwezi ujao , timu nne za juu zitakuwa zimekata tikiti zao kwenda Brazil mwakani wakati timu itakayomaliza nafasi ya tano itapambana na ama Jordan ama Uzbekistan mwezi Novemba ili kupata nafasi moja iliyo wazi.

Kocha aliyeitawaza Bayern Munich kuwa mabingwa wa champions league msimu uliopita , mabingwa wa Bundesliga na kombe la shirikisho DFB Pokal nchini Ujerumani msimu uliopita, Jupp Heynckes ametunukiwa medali ya Fairplay ya shirikisho la soka la Ujerumani, DFB kwa kukiongoza kikosi hicho cha Super Bayern kupata mataji matatu katika msimu mmoja.

Tennis.

bingwa mtetezi Serena Williams aliingia katika fainali ya mchezo wa tennis ya US Open akipambana na Victoria Azarenka wakati wachezaji hao wa juu wakipata ushindi katika michezo yao ya nusu fainali jana. fainali hiyo itakuwa ni marudio ya fainali ambapo wasichana hao walipambana tena katika fainali kama hiyo mwaka uliopita.

Riadha.

Usain Bolt yuko tayari sasa kwenda mapunzikoni baada ya kupata medali nyingine tatu za dhahabu katika msimu mmoja ambapo alishindwa mara moja tu , na hiyo ilikuwa kwa sekunde kiduchu tu.

Mjamaica huyo alishinda mbio za mita 100 kwa kutumia sekunde 9.80 katika ligi ya diamond jana Ijumaa. Mchezaji mwenzake wa Jamaiya Asafa Powell na Tyson Gay wa Marekani waligunduiliwa kuwa wanatumia madawa ya kuongeza nguvu , na kuumia kwa hasimu wake mkubwa kutoka Jamaica Yohan Blake kumewanyima wapenzi wa riadha washindani wao nyota katika riadha.

Mkutano wa kamati ya IOC

Kamati ya kimataifa ya olimpiki IOC, imeanza rasmi kikao chake muhimu za maamuzi jana Ijumaa(06.09.2013) mjini Buenos Aires. Wajumbe wa kamati hiyo wanakabiliwa na majukumu matatu muhimu hadi siku ya Jumanne.

Leo Jumamosi(07.09.2013) wanakabiliwa na uteuzi wa mji mwenyeji wa mashindano ya michezo ya olimpiki ya mwaka 2020 baina ya Tokyo, Istanbul na Madrid. Baadaye wanapaswa kuteua mchezo mmoja katika michezo ya olimpiki , ama mchezo wa Squash, mieleka ama softball ama baseball, na siku ya Jumanne wajumbe watachagua mrithi wa rais wa IOC Jacques Rogge kutoka orodha ya wagombea sita.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / ape / afpe /

Mhariri: Mohammed Dahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW